RAIS MAGUFULI NA WAZIRI MKUU WA ETHIOPIA WAKUBALIANA KUKUZA ZAIDI UHUSIANO NA USHIRIKIANO WA KIUCHUMI
Waziri
Mkuu wa Shirikisho la Kidemokrasia la Jamhuri ya Ethiopia Mhe. Hailemariam
Dessalegn amemhakikishia Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.
John Pombe Magufuli kuwa nchi yake ipo tayari kuimarisha na kukuza zaidi
uhusiano na ushirikiano wake na Tanzania utakaosaidia kuleta manufaa makubwa
zaidi kiuchumi na kukabiliana na umasikini wa wananchi wa nchi zote mbili.
Mhe.
Hailemariam Dessalegn ametoa kauli hiyo jana Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati
akizungumza na wananchi wa Tanzania na Ethiopia kupitia vyombo vya habari muda
mfupi baada ya kuwasili nchini kwa ziara rasmi ya kiserikali ya siku mbili,
anayoifanya kwa mwaliko wa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Miongoni
mwa maeneo ambayo Mhe. Hailemariam Dessalegn alisema atatilia mkazo ni
ushirikiano katika usafiri wa anga ambapo aliahidi kuwatuma wataalamu kutoka
Shirika la Ndege la Ethiopia kuja nchini kushirikiana na Wataalamu wa Shirika
la Ndege la Tanzania (ATCL) ili kuimarisha utendaji kazi na kuikuza ATCL.
“Shirika
letu la ndege la Ethiopia ni shirika linaloendeshwa kwa faida Barani Afrika,
lina ndege 96 na linatarajia kununua ndege nyingine 42, ndege zake zinatua
katika viwanja 92 duniani kote na viwanja 42 ndani ya Ethiopia, hivyo
nitawaleta viongozi wa shirika hili ili waje washirikiane na ATCL kuweka
mkakati wa namna ya kuiendeleza ATCL na kuiwezesha kufanya kazi kwa faida”
alisema Mhe. Hailemariam Dessalegn.
Pia
alisema Shirika la Ndege la Ethiopia kwa kushirikiana na ATCL litaufanya Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam kuwa kituo chake
cha mizigo (Cargo Hub) na hivyo kuwezesha mizigo ya ukanda wa Afrika Mashariki
na maeneo jirani kutumia uwanja huo kusafirisha mizigo yake duniani kote.
Mhe.
Rais Magufuli na Mhe. Hailemariam Dessalegn ambao kabla ya kuzungumza na
wananchi walifanya mazungumzo rasmi, walisema wamekubaliana kuwa Tanzania na
Ethiopia zibadilishane uzoefu juu ya uzalishaji wa nishati ya umeme kwa kutumia
maji ambapo Mhe. Hailemariam Dessalegn aliahidi kuwatuma wataalamu wa nchi yake
kuja nchini Tanzania kutoa uzoefu wa namna Ethiopia ilivyoweza kuzalisha kiasi
kikubwa cha umeme kwa kutumia maji ukiwemo mradi mkubwa unaoendelea kujengwa
uitwao Grand Ethiopian Renaissance Dam (GERD) ambao unatarajiwa kuzalisha
megawatts 6,470 za umeme.
“Mhe.
Waziri Mkuu tutafurahi sana kushirikiana nanyi katika suala la uzalishaji wa
nishati ya umeme kwa sababu hata sisi tunaweza kuzalisha umeme mwingi katika
maporomoko ya maji ya Stiegler’s Gorge yaliyopo katika mto Rufiji” alisema Mhe.
Rais Magufuli.
Viongozi
hao walikubaliana kushirikiana kufanya mapinduzi ya kilimo na mifugo, hasa
ikizingatiwa kuwa Ethiopia inaongoza kwa idadi kubwa ya ng’ombe barani Afrika
na Tanzania inashika nafasi ya pili na kwamba juhudi hizo zitakwenda sambamba
na kujenga viwanda vingi vitakavyoongeza thamani ya mazao.
“Naamini
kuwa tukishirikiana katika kilimo na mifugo, tutaweza kutumia teknolojia za kisasa
katika uzalishaji wa mazao ikiwemo ngozi na nyama na tutatumia mashirika yetu
ya ndege kuyafikia masoko mbalimbali duniani na hivyo kukuza uchumi na
kuwaongezea wakulima wetu kipato” alisisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha,
viongozi hawa walikubaliana kushirikiana kwa kubalishana uzoefu juu ya namna
sekta mbalimbali zitakavyoleta manufaa ya kiuchumi zikiwemo huduma za benki,
madini na gesi, elimu na mawasiliano
hususani simu.
Mhe.
Rais Magufuli alisema ziara ya Waziri Mkuu Mhe. Hailemariam Dessalegn imekuwa
ya manufaa makubwa kwa Tanzania na amesisitiza kuwa wakati umefika wa kukuza
biashara kati ya nchi hizi ambazo kwa sasa thamani ya biashara kati yake ni
Dola za Marekani milioni 2.24 tu.
Kabla
ya kuzungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari, viongozi hao walishuhudia
utiaji saini wa mikataba 3 ambayo ni Mkataba wa Mkakati wa ushirikiano kati ya
Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ethiopia, Mkataba wa kuanzishwa Kamisheni
ya Pamoja ya Kuduma kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ethiopia na
Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya utalii kati ya Serikali ya
Tanzania na Serikali ya Ethiopia.
Waziri
Mkuu wa Shirikisho la Kidemokrasia la Jamhuri ya Ethiopia Mhe. Hailemariam
Dessalegn aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
Jijini Dar es Salaam jana asubuhi na kupokewa na mwenyeji wake Mhe. Rais
Magufuli aliyeongozana na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na akiwa
uwanjani hapo alipigiwa mizinga 19, alikagua gwaride lililoandaliwa kwa heshima
yake na alishuhudia burudani ya ngoma za asili.
No comments