HAYA NI MAENEO 5 YANAYOKUMBWA NA MAFURIKO JIJINI DAR ES SALAAM KILA MWAKA

Kama sio mwenyeji wa
jiji la Dar es Salaam basi ni vema ukauliza kwanza kabla ya kuhamia
sehemu na kuanza kuishi. Usipofanya hivyo kwenye kipindi cha mvua kama hiki
usishangae unaamka ukiwa umezungukwa na maji kama sio kuelea kabisa.
Kuwa na vipindi virefu vya jua na joto kali haimaanishi kuwa
maeneo yote ya Dar es Salaam hubakia hivyo mwaka mzima. Jumia Travel
imekusogezea maeneo haya 5 ambayo miaka nenda rudi lazima yakumbwe na
mafuriko.
Jangwani
Umaarufu wa Jangwani ni kwamba mvua ikinyesha tu, bila hata ya
kutazama taarifa ya habari utajua ni lazima mafuriko yamelikumba eneo hilo. Na
hii yote ni kutokana na jiografia ya eneo hili kupakana na mto Msimbazi ambao
hupokea maji kutoka mito mbalimbali jijini Dar es Salaam kuelekea bahari ya
Hindi ambayo ipo mita chache tu. Kwa muda mrefu wakazi wa eneo hili wamekuwa
wakiambiwa na serikali kuhama lakini wamekuwa ni wakaidi. Sababu kubwa
inayowafanya wakazi wengi kuling’ang’ania eneo hili ni kwa sababu lipo karibu
na katikati ya jiji pamoja na huduma lukuki za kijamii kama vile usafiri.
Wakazi wengi wanaoishi eneo hili hutembea kwa miguu kufika maeneo ya kazi.

Tandale
Kutokana na msongamano mkubwa wa makazi ya watu imekuwa ni
vigumu sana kwa maji kupita kwenye njia yake. Kwa kiasi kikubwa eneo hili lipo
kwenye mkondo wa maji na ndio sababu inayopelekea kukumbwa kwa urahisi na
mafuriko. Urahisi wa upatikanaji na unafuu wa vyumba vya kupanga katika eneo
hili usikudanganye na kujikuta ukataka kuishi. Siku zote nafuu ni gharama kama
walivyosema wahenga. Ni kweli maisha ya Tandale ni ya chini sana lakini
nakuhakikishia gharama utakazokuja kuingia kipindi cha mafuriko utajuta
kulifahamu hilo eneo.

Buguruni kwa Mnyamani
Eneo la Buguruni lipo kwenye Wilaya ya Ilala ambayo ni maarufu
kwa shughuli mbalimbali za kibiashara kama vile masoko ya Karume, Buguruni na
Kariakoo. Ikiwa imezungukwa na biashara mbalimbali pamoja na huduma lukuki za
kijamii, sio Buguruni yote ni mahali salama kwa makazi ya watu. Ikifika kipindi
cha mafuriko Buguruni nayo huingia kwenye anga za habari za waathirika hususani
eneo la kwa Mnyamani. Eneo hili kama maeneo mengine yanayokumbwa na mafuriko,
wakazi wamejenga kwenye vyanzo vya maji na kuviziba kabisa.
Kuna athari kubwa sana za kuzuia njia ya maji kwani yakifurika
huwa hayachagui mahali pa kupita. Hivyo basi usije ukarogwa ukakubali kwenda
kuishi eneo hili hata kama chumba ni bure.

Msasani Bonde la Mpunga
Kutokana na ukaribu wake na katikati ya jiji, eneo hili
limevutia uwekezaji mkubwa wa majengo kadhaa ya kibiashara kama vile hoteli,
maduka makubwa ya bidhaa, migahawa, ofisi, kumbi za filamu na mikutano, na
kadhalika. Kwa asilimia kubwa wakazi wa eneo hili ni mchanganyiko wa maisha
duni na wa hali ya kati.
Eneo hili nalo ni sehemu ambayo miaka yote hukumbwa na mafuriko na sababu kubwa
ni kwamba eneo hili lina asili ya majimaji. Sababu pekee ambazo zinawafanya
watu kung’ang’ania eneo hili licha ya mafuriko ni upatikanaji wa huduma
mbalimbali za kijamii, uwepo wa vitega uchumi vingi hivyo kutoa fursa za ajira
lakini pia ni takribani kilometa 6 mpaka kufika katikati ya jiji. Hivyo endapo
utakwenda kuishi eneo hili tegemea kwamba kila ifikapo kipindi cha mvua basi
ujue mafuriko ni lazima.
Bonde la Mto Kigogo
Eneo kubwa la Kigogo limepakana na mto Kigogo ambao hupokea maji
kutoka mifereji mbalimbali na kisha kuungana na mto Msimbazi ambao humwaga maji
yake katika bahari ya Hindi. Kutokana na wakazi wengi kujenga pembezoni mwa mto
huu, ni jambo la kawaida ikifika kipindi cha mvua kukumbwa na mafuriko.
Mvua zikiwa kubwa sana mto hutapika kwenye kingo zake na
kusambaa eneo la karibu yake ambalo kwa kiasi kikubwa limevamiwa na makazi ya
watu. Wakazi wa eneo hili ni mchanganyiko wa maisha ya chini na ya kati mbali
na hapo pia ni karibu kufika katikati ya jiji ukiwa unaishi Kigogo.
Kama utakuwa umegundua
kitu ni kwamba wakazi wengi katika maeneo yaliyotajwa hapo juu wana sababu
zinazofanana. Wengi wameng’ang’ania maeneo hayo kutokana na upatikanaji wa
huduma za kijamii, unafuu wa maisha pamoja na ukaribu wa katikati ya jiji
ambapo ndipo hufanyia shughuli zao. Lakini hizo hazitoshi kuwa sababu za
kuhatarisha maisha yako, Jumia Travel inakushauri kwamba siku zote huduma za
kijamii huwafuata watu na sio kinyume chake.
No comments