SAKATA LA MALIPO YA WADAIWA WA ELIMU YA JUU KUKATWA ASILIMIA 15, TUCTA YATOA SIKU 14 KWA SERIKALI KUWARUDISHIA WAFANYAKAZI FEDHA WALIZOKATWA KINYUME NA MKATABA WA 8%.
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA),
limetoa siku 14 kwa Serikali kurejesha fedha za makato ya mikopo ya asilimia 15
zilizokatwa kikamakosa kupitia Bodi ya Mikopo, likisema sera inayotumika imejaa
utata.
Akizungumza
jana Dar es Salaam, Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya, alisema Serikali lazima irekebishe sheria hiyo ya
Bodi ya Mikopo kupitia Wizara ya Elimu, Teknolojia na Ufundi Stadi kutokana na
kuwajumuisha wafanyakazi wote katika makato ya asilimia 15 wakati imetungwa
hivi karibuni.
Nyamhokya
alisema kuwa wakati sheria hiyo inatungwa, baadhi ya wafanyakazi
walikwishaingia makubaliano mengine ya kukatwa asilimia 8 katika mishahara yao.
Alisema
wamesikitishwa na hatua hiyo ya Serikali, ingawa wanaamini haitalifumbia macho
suala hilo.
Aidha
Nyamhokya alisema kuna milolongo mingi ya makato katika mishahara ya
wafanyakazi ambayo ni zaidi ya asilimia 57, huku pia mazingira ya kufanyia kazi
yakiendelea kuwa magumu na Serikali ikishindwa kuongeza mishahara wala
kuwapandisha vyeo kwa muda mrefu.
Aidha
alisema kwa kawaida mtumishi mwenye mkopo serikalini analipa kwa makubaliano
maalumu, lakini mtindo wa bodi hiyo kukusanya fedha za wanufaika kabla ya
kuanza kwa sheria husika kumeleta athari kwa watu wengine.
No comments