ZIFAHAMU FAIDA ZITOKANAZO NA RASILIMALI ZA BONDE LA MTO NILE KWA TANZANIA
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Mto
Nile ni miongoni mwa mito mikubwa iliyopo upande wa Mashariki ya Bara la Afrika
na Duniani kote ukiwa na urefu wa kilomita 6,695 ambapo beseni ya Nile
hukusanya maji ya eneo linalojumuisha 10% za eneo la Afrika yote.
Kwa
muonekano wa juu Mto Nile unaonekana kama pembetatu wakati upande wa chini wa
eneo la Nile (Kaskazini) na upande wa juu (Kusini) kuna mimea mbalimbali
inayoota kwa wingi pia katika kipindi cha mwisho wa mwaka eneo la mto Nile huwa
linakuwa na mwonekano mwekundu na kuwa na maua yanayojulikana kama lotus
flowers.
Japokuwa
mimea hii haioti kwa wingi wakati huu kama ilivyokuwa hapo awali, mimea
inayoota kwa wingi katika eneo la Mto Nile kwa upande wa chini ni yale
yanayojulikana kama Egyptian lotus na kwa upande wa juu hujawa na mimea inayoitwa
Cyperus papyrus.
Chemchemi
za Nile ni mito yote inayopeleka maji kwenda Ziwa Viktoria katika nchi za
Tanzania, Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda na Kenya na
kwa upande mwingine wa Nile unaanzia Ethiopia ukiitwa Abbai au Nile ya Buluu
unatoka katika Ziwa Tana wakati chanzo cha mbali kabisa ni mto wa Luvironza
huko Burundi unaoingia katika mto wa Kagera na kufika Ziwa Viktoria.
Mto
huo ambao unaanzia Ziwa Victoria nchini Tanzania, ni chanzo kikubwa cha maji kwa ajili ya matumizi ya
nyumbani, viwandani, kilimo cha umwagiliaji na kuzalisha umeme kwa wakazi wa
nchi za bonde hilo.
Kutokana
na nchi nyingi kuzungukwa na mto Nile, suala la ushirikiano katika kusimamia na
kuendeleza rasilimali za Bonde la Mto huo limepewa kipaumbele ili kuzuia
migogoro inayoweza kuzuka baina ya nchi ambazo wanatumia mto huo.
Mkurugenzi
Mtendaji wa taasisi inayosimamia shughuli za wanachama wa Bonde la Mto Nile
(NBI), Innocent Ntabana anasema kuwa azma ya kusimamia na kuendeleza rasilimali
za Bonde la Mto Nile limepewa kipaumbele na nchi zote zinazozungukwa na mto
huo, jambo hilo ndilo limesababisha kuanzishwa kwa Sekretarieti ya NBI mwaka
1999 jijini Dar es Salaam.
“NBI
ina jukumu la kusimamia na kuendeleza rasilimali za maji za Bonde la Mto Nile kwa
niaba ya nchi wanachama zipatazo 10 ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda,
Burundi, Ethiopia, Sudan, Sudan ya Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na
Misri,” anasema Ntabana.
Kwa
upande wa Mratibu wa Kanda wa Kitengo cha Uratibu cha Bonde la Mto Nile
(NELSAP-CU), Elicad Nyabeeya anasema kuwa mto huo una manufaa makubwa kwa nchi
wanachama kwani muunganiko wa nchi hizo umeleta mawasiliano mazuri ambayo
yanapelekea kuinua uchumi wa nchi hizo pia kwa upande mwingine uwepo wa
ushirikiano huo umesaidia nchi wanachama kufahamu tamaduni za watu tofauti
tofauti.
Nyabeeya
anakaririwa akisema kuwa “Nchi ya Tanzania inafaidika kutokana na uwekezaji
mkubwa uliofanywa na NBI kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo
miradi ya ujenzi wa bwawa la Bisrawi na usanifu wa bwawa la Borenga, mkoani
Mara”.
Kwa
mujibu wa Nyabeeya, nchi hii itanufaika na miradi ya maji na nishati ya umeme,
pamoja na miradi mingine mingi ambayo NBI inaendelea kuitekeleza kama vile
ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa Rusumo na umwagiliaji katika mabonde ya
mito Kagera na Ngono iliyopo mkoani Kagera.
Anaendelea
kufafanua kuwa mradi wa umeme wa Rusumo utazalisha megawati 80 za umeme ambazo
zitatumiwa na nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi ambapo Tanzania inatarajiwa
kupata megawati 16.
Miradi
mingine ni ya kuunganisha umeme kutoka Ethiopia, Kenya hadi Tanzania, mradi wa
umeme kati ya Tanzania na Zambia.
Aidha,
NBI wanatarajia kukamilisha upembuzi yakinifu wa kina wa miradi ya Mara na
Ngono ifikapo mwezi Aprili mwaka huu ambapo wananchi 20,000 pamoja na hekari
13,630 katika vijiji 21 vinatarajiwa kunufaika na mradi wa Ngono wakati Bonde
la Mara litanufaisha wanachi 10,000. Miradi hiyo itahusisha usambazaji wa maji
kwa ajili ya matumizi ya majumbani, mifugo na shughuli za umwagiliaji.
Wakati
huo, Bwawa la Borenga litakuwa likisambaza maji katika Bonde la Mara kwa wakazi
wa vijiji 13 kwa ajili ya umwagiliaji na 17 vitapata maji kwa ajili ya matumizi
ya nyumbani na mifugo.
Madhumuni
ya miradi hiyo ni kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa maji ya uhakika,
kuimarishwa kwa soko na mahusiano na kukuza sekta binafsi, kilimo, usalama wa
chakula na kupunguza umaskini.
Kutokana
na kuwepo kwa umuhimu wa rasilimali za Bonde la mto huo, iliamuliwa kuwa
Februari 22 ya kila mwaka iwe ni siku rasmi ya kuadhimisha uanzishwaji wa
muunganiko wa matumizi ya pamoja ya rasilimali za mto huo baina ya nchi 10
wanachama .
Mkurugenzi
Msaidizi wa Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Mhandisi
Sylvester Matemu amesema kuwa lengo la Siku ya Nile ni kukuza uelewa kwa watu
wote kuhusu umuhimu wa ushirikiano baina ya nchi zote wanachama, masuala
yanayotekelezwa na faida inayopatikana kutokana na matumizi bora ya rasilimali
za Bonde la Mto huo.
“Maadhimisho
ya siku ya Nile kuadhimishwa katika nchi fulani ni tukio la kihistoria
kwasababu ni tukio ambalo halifanyiki katika nchi moja kila mwaka hivyo kwa
vile nchi wanachama tuko 10 basi
linatokea mara moja kila baada miaka 10,”anasema Mhandisi Matemu.
Maadhimisho
ya 11 ya Siku ya Nile kwa mwaka huu yameadhimishwa nchini Tanzania kwa
ushirikiano wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji pamoja na Sekretariati ya Nile
Basin Initiative (NBI) ambapo mgeni rasmi wa maadhimisho hayo alikuwa Makamu wa
Rais, Samia Suluhu Hassan na kuhudhuriwa na watu zaidi ya 600 wakiwemo Mawaziri
wa nchi wanachama kutoka kwenye nchi husika, mabalozi mbalimbali, wabunge, watu
kutoka taasisi na mashirika mbalimbali pamoja na wanafunzi wa shule za Msingi,
Sekondari na Vyuo Vikuu.
Shughuli
hizo zilianza kwa maandamano yaliyoongozwa na Bendi ya Polisi kuanzia Viwanja
vya Mnazi Mmoja hadi Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere ambako
maonesho pamoja na ufunguzi rasmi wa maadhimisho hayo vilifanyika.
No comments