SEKRETARIETI YA AJIRA YATOA ELIMU YA MASUALA YA AJIRA KWA WANAFUNZI WA VYUO ZANZIBAR
Na Kassim Nyaki-PSRS
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa
Umma imefanya ziara katika Vyuo Zanzibar ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa
utaratibu wake wa kuhamasisha na kuelimisha wanafunzi wa Vyuo mbalimbali nchini
kuhusu utaratibu wa uendeshaji wa mchakato wa Ajira katika Utumishi wa Umma.
Ziara hiyo ambayo ilifanyika kwa
ushirikiano kati ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma na Ofisi ya
Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Zanzibar ililenga kutoa
hamasa na elimu kwa wanafunzi wa Vyuo kama sehemu ya wadau katika mchakato wa
Ajira.
Katika ziara hiyo mada mbalimbali zimeweza
kutolewa kwa wanafunzi hao ikiwemo taratibu za uendeshaji wa Mchakato wa Ajira
katika Utumishi wa Umma na changamoto zake, Masharti ya msingi ya kuzingatiwa
kabla na baada ya kuwasilisha maombi ya kazi, Matumizi ya TEHAMA hususani namna
ya kujisajili katika mfumo wa maombi ya kazi.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira Bibi Riziki Abraham akiongea na wanafunzi
wa Vyuo mbalimbali alibainisha kuwa mada hizo zimelenga kutoa uelewa kwa
wanafunzi wa Vyuo ili waweze kujua majukumu ya Sekretarieti ya Ajira, taratibu
za kufuata kabla ya kuomba ajira Serikalini, namna ya kujiandaa kabla na wakati
wa usaili pamoja na utaratibu wa uwasilishaji wa maombi ya kazi kwa njia ya
mtandao ujulikanao kama Recruitment portal.
“Wanafunzi wa vyuo kama sehemu ya wadau
wetu wakubwa katika masuala ya ajira ni mategemeo yetu kuwa mtakapohitimu
masomo yenu mtaingia kwenye soko la ajira, hivyo ni vizuri mkafahamu taratibu
za kuomba kazi, namna ya kuandaa wasifu binafsi (CV) namna ya kuandika barua za
maombi ya kazi, jinsi ya kujiandaa kabla na wakati wa usaili na utaratibu mpya
wa utumaji na upokeaji wa maombi ya kazi kwa njia ya Mtandao ujulikanao kama
Recruitment portal” ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuweza kushindana
katika soko la ajira nchini, alisisitiza Riziki.
Vyuo Vikuu vilivyotembelewa ni pamoja na
Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar-SUZA, Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Tawi
la Zanzibar, Chuo cha Utumishi wa Umma Zanzibar pamoja na Chuo Kikuu cha
Sumait.
Aidha, ziara hiyo pia ililenga kutoa uelewa
kwa wanafunzi wa Vyuo kuzifahamu Wizara na Taasisi zinazotekeleza masuala ya
Muungano ambapo katika mchakato wa Ajira kwa Wizara na Taasisi hizo waombaji
kazi kutoka Tanzania Bara wanapata asilimia 79 na waombaji kazi kutoka Zanzibar
asilimia 21 ya mgao wa Ajira kwenye Wizara na Taasisi hizo za Muungano.
Mkurugenzi wa Mipango na Rasilimali watu
kutoka Wizara ya Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Zanzibar Bw.
Hamis Haji Juma wakati akizungumza na wanafunzi wa vyuo hivyo alibainisha kuwa
ziara hiyo imesaidia kuwaelimisha wanafunzi kujua fursa za Ajira kwa upana wake
ikiwa ni pamoja na waombaji kazi kutoka Zanzibar kuomba nafasi za kazi
zinatotangazwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Ajira
zinazotangazwa kupitia Wizara na Taasisi zenye masuala ya Muungano.
Ziara hiyo pia imetumika kuwafahamisha
wadau mbalimbali ikiwemo wanafunzi wa Vyuo hivyo juu ya uwepo wa Ofisi ya
Sekretarieti ya Ajira katika eneo la Shangani Zanzibar ambayo itasaidia
kuboresha utendaji kazi na kuratibu masuala mtambuka yanayohusiana na
uendeshaji wa mchakato wa Ajira katika Utumishi wa Umma hasa katika Wizara na
Taasisi za Muungano..
No comments