MHE SAMIA SULUHU: MAJAJI NA MAHAKIMU WANAWAKE KUHAKIKISHENI MNAPAMBANA IPASAVYO KATIKA KUKABILIANA VITENDO VYA RUSHWA NA UNYANYASAJI WA KIJINSIA.
Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaagiza majaji na
mahakimu wanawake kote nchini kupambana ipasavyo katika kukabiliana vitendo vya
rushwa,unyanyasaji kijinsia na rushwa ya ngono ili kusaidia wanawake kupata
haki zao za msingi bila kubaguliwa katika jamii.
Makamu wa Rais Samia
Suluhu Hassan ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam wakati anafungua Mkutano
Mkuu wa NANE wa Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake Tanzania (TAWJA).
Makamu wa Rais pia
ameonya kuhusu vitendo vya rushwa ya ngono inayofanywa na baadhi ya watendaji
wenye madaraka na kusema tabia hiyo ni mbaya na lazima ikomeshwa mara moja
katika jamii.
Amesema kuwa vitendo hivyo vya rushwa ya ngono
huzuia na kukwamisha juhudi za wanawake kufikia huduma za kijamii na za
kiserikali ipasavyo ikiwemo elimu, ajira na haki kwa ajili ya ustawi wa
wanawake.
Aidha Makamu wa Rais
Samia Suluhu Hassan amekishukuru Chama cha Dunia cha Majaji Wanawake (IAWJ) kwa
mchango na msaada wake kwa TAWJA katika programu ya miaka mitatu ya kupambana
na matumizi mabaya ya madaraka na rushwa ya ngono.
Makamu wa Rais pia
ameipongeza Wizara ya Katiba na Sheria, Shirika la UN Women na wadau wengine wa
TAWJA kwa kuunga mkono mapambano ya aina zote za ubaguzi na ukatili dhidi ya
wanawake na watoto nchini.
Amesema elimu ya haki
za Binadamu iliyotolewa na Chama hicho imeleta badiliko kwa wengi kwa njia ya
mafunzo na machapisho na jitihada hivyo lazima ziongezwe ili huduma hiyo iweze
kuwafikia wananchi wengi zaidi kote nchini.
Amesisitiza wanachama wa Chama cha TAWJA
waendelee kutoa msaada katika kuwasaidia wanawake na watoto ambao
wanakandamizwa kwa kunyimwa haki zao katika jamii ili waweze kupata haki zao
nchini.
Kwa upande wake, Jaji
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mohamed Chande Othman amemhakikishia
Makamu wa Rais kuwa mkakati wa uimarishaji wa shughuli za mahakama nchini
unaendelea vyema lengo likiwa ni kutenda haki kwa wananchi kote nchini bila
ubaguzi.
Kauli mbiu ya Mkutano
Mkuu wa NANE wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (TAWJA) “Kuongoza njia
kufikia hitajio la upatikanaji wa haki kwa wote na kwa wakati”.
No comments