MAZOMBI YAVAMIA OFISI ZA CUF ZANZIBAR, YAPORA MALI NA KUJERUHI WATU
Watu
wasiojulikana maarufu kama mazombi wameivamia ofisi ya Chama cha Wananchi (CUF)
katika Jimbo la Dimani Wilaya ya Magharibi B.
Katika
tukio hilo lililotokea saa 6.30 usiku wa kuamkia jana, inadaiwa mazombi hayo
yalipora mali, kujeruhi watu na kuwateka wengine wa nyumba jirani na ofisi
hiyo.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassan Nassir Ali alithibitisha kuwepo kwa
tukio hilo huku CUF wakitaka uchunguzi uanze mara moja kuwabaini wahalifu.
“Ni kweli taarifa tunazo za watu kuvamia ofisi
hiyo ya CUF na kuwapiga pamoja na kuwahujumu watu na huo ni uharamia
unaoripotiwa mara kwa mara,” alisema Kamanda Ali.
Katika
tukio hilo, watu hao walioripotiwa kuwa na bunduki na silaha za jadi kama
mashoka, mapanga, mashanuo, chupa, spoku za baiskeli na nyundo, walidaiwa
kuvunja milango ya jengo la ofisi hiyo katika kijiji cha Bweleo kabla ya
kutembeza kipigo kwa majirani na kuondoka na vitu kadhaa.
Katika
tukio hilo inadaiwa mazombi walitoweka na watu kadhaa akiwamo Mwenyekiti wa CUF
Tawi la Bweleo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazee wa chama hicho
Wilaya ya Magharibi, Juma Ali Juma.
Akilaani tukio hilo, Mkurugenzi wa Habari,
Uenezi na Mahusiano ya Umma wa CUF, Salim Abdallah Bimani alisema, “Huu ni
uvunjifu wa amani na tunataka Rais John Magufuli iwapo anayo nia ya dhati
afuatilie hujuma hiyo ambayo watekelezaji wake wanajulikana lakini
hawakamatwi.”
Bimani
alisema, “Mazombi wameshawapiga sana wananchi hasa wafuasi wa CUF ambao hawana
hatia, wengine mpaka walipo-teza maisha, wameshawapiga watu na kuwajeruhi
vibaya na pia kuwaibia watu mali zao na hatuoni hatua yoyote ikichukuliwa.”
Bimani
alisema, “Tunamwambia Rais Magufuli kwa mujibu wa Katiba yeye ndiye mwenye
mamlaka ya kuwalinda raia wote wa nchi hii, achukue hatua.”
Naibu
Mkurugenzi wa Haki za Binadamu wa CUF, Pavu Juma Abdalla aliwataja
waliojeruhiwa kutokana na vipigo vikali kuwa ni pamoja na Juma Shani Mwita, Ali
Saleh Shani, Kessi Khatib na Ame Mahmoud, wote wakazi wa Bweleo.
Pavu
alisema kuwa tukio hilo liliripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Fumba na
wahusika walipewa RB Na.18/2017.
Kwa
mujibu wa Mkurugenzi huyo inadaiwa kuwa miongoni mwa mali walizotoweka nazo
‘mazombi’ kutoka ndani ya ofisi hiyo, ni simu nne, fedha taslimu Sh300,000,
viti 20, kifaa cha kudhibiti umeme, friji na bendera na mlingoti wake.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassan Nassir Ali alisema, “Ni kweli taarifa
tunazo za watu kuvamia ofisi hiyo ya CUF na kuwapiga pamoja na kuwahujumu watu
na huo ni uharamia unaoripotiwa mara kwa mara.”
Nassir
alisema, “Pamoja na juhudi tunazozichukua ili kuukomesha kwa kushirikiana na
vikosi vingine, inaonekana hauwezi kuondoka kwa mara moja.”
Alisema
kuwa jana walifanikiwa kuwashikilia watu wawili ili kusaidia polisi wakati
ambapo jeshi hilo likiendelea na upelelezi.
Shambulio
hilo lilitendeka saa chache baada ya makamu mwenyekiti mstaafu wa CUF, Juma
Duni Haji na Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea kuwasili Dimani ili
kuendelea na kampeni za kumnadi mgombea wao, Abdulrazaq Khatib Ramadhan.
No comments