MAALIM SEIF NA LOWASSA KUTIKISA ZANZIBAR KESHO KUFUNGUA PAZIA LA KAMPENI JIMBO LA DIMANI
Wanasiasa
wakongwe nchini, Maalim Seif Sharif Hamad aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar na Edward Lowassa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania katika, kesho wanatarajia kuungana kwa mara ya kwanza jukwaani tangu
kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Vigogo
hao wa vyama vya CUF (Maalim Seif) na Chadema (Lowassa) wataunguruma katika
viwanja vya Skuli ya Fuoni visiwani Zanzibar kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la
Dimani kwa tiketi ya CUF, Abdulrazaq Khatib Ramadhani, katika uchaguzi mdogo
utakaofanyika Januri 22 kuziba nafasi ya aliyekua mbunge wa jimbo hilo, Hafidh
Ally Tahir aliyefariki dunia Novemba 11 mwaka jana.
Naibu
Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu amesema kuwa chama chake kimemua kuungana
na CUF katika uchaguzi huo ili kuhakikisha mshirika wake huyo wa Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) anamshinda mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aidha,
Mwalimu aliongeza kuwa baada ya Lowassa kushiriki uzinduzi wa kampeni hizo
kesho, viongozi wengine wa Chadema watafuata kwa kufanya mikutano mbalimbali
jimboni humo. Alisema kuwa baada ya Lowassa atafuata Mwenyekiti wa chama hicho,
Freeman Mbowe pamoja Tundu Lissu kwa nyakati tofauti, kisha wengine wataendelea
hadi mwisho wa kampeni hizo.
Akizungumzia
uamuzi huo wa Chadema, Mkurugenzi wa Habari,Uenezi na Mawasiliano kwa Umma,
Salim Bimani alieleza kufurahishwa na uamuzi huo wa Chadema na kueleza kuwa
hatua ya Lowassa kuhudhuria uzinduzi huo itaongeza hamasa kubwa kwa wapenzi wa
chama hicho.
“Umenambia
hadi Lowassa atakuwepo? Ni furaha iliyoje, Wanzibari wana shauku kumuona. Siku
ya kampeni patakuwa hapatoshi Skuli ya Fuoni, hapa Simba (Maalim Seif) kule
Lowassa kipenzi kingine cha Wazanzibar,” Bimani anakaririwa na Mwananchi.
Aliongeza
kuwa kama Lowassa atahudhuria mkutano huo atakuwa na mambo mawili makubwa ya
kufanya, la kwanza likiwa kuwashukuru Wazanzibar kwa kura walizompa katika
uchaguzi Mkuu wa mwaka jana. Na la pili litakuwa kumpigia kampeni mgombea wa
CUF, Abdulrazaq Khatib Ramadhani.
Lowassa
ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu
wa CUF, wataingia katika jimbo hilo ikiwa ni siku chache baada ya Katibu Mkuu
wa CCM, Abdulrahman Kinana kufanya uzinduzi wa kampeni hizo akiambatana na
viongozi wengine wa kitaifa wa chama hicho.
Hivyo,
kwa muktadha wa kisiasa, vigogo hao wa Ukawa wana kazi ya kusawazisha matuta
yaliyowekwa na timu ya chama tawala iliyoongozwa na Kinana.
No comments