KUTOKA KONDOA: ASKARI 3 KIKOSI CHA WANYAMA PORI MBARONI KWA KUUA NA KUFICHA MAITI
Jeshi
la polisi mkoani Dodoma, linawashikilia askari watatu wa wanyamapori wa pori la
akiba Swagaswaga wilayani Kondoa, wakituhumiwa kumuua mkazi wa kijiji cha
Olimba wilaya ya Chemba kwa kumpiga risasi mgongoni wakimtuhumu kubeba nyama
pori.
Akizungumza
ofisini kwake leo, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Lazaro Mambosasa, alisema
tukio hilo lilitokea Disemba 31,mwaka jana saa 7:30 mchana katika kijiji cha
Selya kata ya Selya wilayani humo.
“Marehemu
ambaye hakufahamika jina lake lakini mkazi wa kijiji hicho, alikuwa akiendesha
pikipiki huku akiwa amepakia kiroba kilichokuwa na sukari guru ndani yake,
lakini askari wanyamapori hao walimhisi amebeba nyama pori na bila kumsimamisha
na kumhoji waliamua kutumia bunduki zao kumuua papo hapo,” alisema Kamanda
Mambosasa.
Aidha
Kamanda huyo amesema baada ya kufanya mauaji hayo, askari hao waliubeba mwili
huo kwenye gari walilokuwa nalo pamoja na pikipiki ya marehemu na kiroba cha
sukari guru, kisha kwenda kuutelekeza mwili huo ndani ya pori hilo la
Swagaswaga.
“Baada
ya kuutelekeza mwili huo ndani ya pori hilo, walichukua pia pikipiki na kiroba
na kuvificha kila kimoja mahali pake kwa lengo la kupoteza ushahidi wa tukio
hilo”.
Kamanda
Mambosasa alisema wakati askari hao wanafanya tukio hilo, walishuhudiwa na
mwananchi mmoja wa kijiji hicho ambaye alijificha porini ambaye aliamua kutoa
taarifa kituo cha polisi Kondoa.
Wahusika
wa tukio hilo ambao wanaendelea kuhojiwa
kabla ya kufikishwa mahakamani ni George Grefee (26), Chini Paulo (40) na
Christopher Waunko (36).
No comments