KUFATIA KUWEPO TAARIFA MTOTO KUFARIKI WAKATI WAKIKEKETWA, POLISI KUFUKUA KABURI LA MTOTO HUYO ALIYEZIKWA KWA SIRI ARUSHA,
FAMILIA
jijini Arusha inadaiwa kumzika kwa siri mtoto wao mdogo wa kike wa miaka mitatu
katika kaburi lililofichwa, huku majirani wakidanganywa kuwa binti huyo yupo
hai.
Taarifa
za kisa hicho cha kusikitisha zimevifikia vyombo vya usalama. Kwa sasa kuna
mipango ya kuhakikisha kuwa mwili wa binti huyo, Nuru Losipha aliyezikwa kwa
siri na familia yake, unafukuliwa kwa uchunguzi zaidi.
Inadaiwa
kuwa Losipha alipoteza maisha wakati akifanyiwa tohara au ukeketaji na ngariba,
ambaye jina lake halikufahamika mara moja, huku familia yake ikishuhudia.
Kitendo
hicho kilifanyika katika kijiji cha Engutoto Kata ya Mwandeti wilayani Arumeru
Desemba 28, mwaka jana, zikiwa zimebaki takriban siku tatu tu, kabla ya mtoto
huyo aliyekuwa na umri wa miaka mitatu tu, hajaingia mwaka mpya wa 2017.
Mtendaji
wa Kata ya Mwandeti, Njivaini Kivuyo awali alikuwa amepitwa na taarifa hizo
hadi vyombo vya habari vilipotinga kijijini hapo kwa uchunguzi na ndipo
alipolazimika kwenda kuripoti tukio hilo kwenye kituo cha Polisi cha
Ngaramtoni.
Kamanda
wa Polisi mkoani hapa, Charles Mkumbo aliapa kuwa liwalo na liwe na kwamba
ikiwezekana kaburi litafukuliwa ili mwili wa malaika huyo asiye na hatia,
uchunguzwe upya.
“Ndio
kwanza nazipata hizi taarifa, na kama polisi tutaomba kibali cha mahakama ili
twende kulifukua kaburi husika tujiridhishe kama kweli mtoto huyo amezikwa humo
na iwapo tutaukuta huo mwili, basi tutaanza uchunguzi juu ya kifo chake,”
alisema Kamanda arles Mkumbo.
Baba
wa marehemu, Losipha Kaiser anadai kuwa mtoto wake alifariki kutokana na
ugonjwa wa baridi yabisi na kwamba aliugua kwa kipindi kirefu kabla ya kupoteza
maisha Desemba 28, mwaka jana. Lakini madai yake hayo yanapingana na ripoti ya
muuguzi katika duka la dawa lililopo kijiji cha jirani cha Kidali, anayeitwa
Jane Andrew.
“Walimleta
mtoto hapa walitaka nimsaidie tiba, lakini tayari huyo binti alikuwa amezimia
na kutokwa na damu nyingi,” alidai.
Muuguzi
huyo aliwahimiza wamkimbize mtoto hospitali, na hakufahamu nini kiliendelea
hadi ripoti za kifo zilipomfikia.
Huku
serikali ikipiga marufuku vitendo vya ukeketaji kwa wasichana, bado kuna
familia nyingi kwenye mikoa ya Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa,
zinaendeleza mila hiyo kwa siri.
Kwa
sasa familia hizo zimegundua mbinu mpya ya kuwatahiri watoto wa kike wakiwa
wadogo sana, kuepuka kukamatwa.
Ngariba
wanaotumika kukeketa watoto, mara nyingi ni akina mama vikongwe wasiokuwa na
ujuzi, taaluma za afya na hutumia vifaa butu, ambazo husababisha uvujaji mwingi
wa damu na kuwa chanzo cha maambukizi ya magonjwa mengine.
Chanzo-Habarileo
No comments