UMEYA WA KINONDONI, CHADEMA WAZUA MVUTANO NA OFISI YA MKURUGENZI
Wakati
mchakato wa uchaguzi wa meya na naibu wake ukiendelea, suala la idadi
ya madiwani wa viti maalumu wa Chadema katika Manispaa ya Kinondoni
limeibua mvutano mpya kati ya chama hicho na ofisi ya mkurugenzi
mtendaji.
Mvutano
huo umejitokeza baada ya Mkurugenzi wa Kinondoni, Aron Kagurumjuli
kutoa barua inayoeleza kuwa kutakuwa na madiwani viti maalumu wanawake
wasiopungua theluthi moja ya madiwani wa kuchaguliwa wa Chadema.
Kwa
mantiki hiyo, Chadema ambayo ina madiwani wa kuchaguliwa saba itakuwa
na madiwani watatu wa viti maalumu. Kwa hiyo majina yasiyopungua matatu
ndiyo yatakayowasilishwa kuunda baraza jipya la madiwani.
Hata hivyo, Katibu wa Chadema Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kilewo alipinga maelezo hayo ya mkurugenzi akisema: “Tayari
nimeshamwandikia barua mkurugenzi kumweleza. Tungekuwa tunatoka katika
uchaguzi mkuu ningekubaliana na hoja ya Kagurumjuli, lakini kwa hali
ilivyo sasa siwezi kukubaliana naye kwa sababu baraza likiitishwa
madiwani hawatakula kiapo kama awali.”
Kuhusu madai hayo Kagurumjuli alisema: “Nasimamia
sheria, sifuati matakwa ya mtu. Nadhani wao wanapingana na sheria.
Sielewi presha inatoka wapi. Wa kushinda atashinda na wa kukosa atakosa
kulingana na idadi ya wajumbe wake na hakuna atakayeonewa.”
Alisisitiza
kuwa kulingana na sheria hiyo na idadi ya madiwani wa kuchaguliwa wa
Chadema, chama hicho hakiruhusiwi kuongeza diwani mwingine. Kagurumjuli
hakuwa tayari kutaja idadi ya wajumbe watakaounda baraza la madiwani na
kusema kwamba anasubiri majina ya madiwani kutoka CUF, Chadema na CCM.
Lakini
Kilewo alisema msimamo wa Chadema uko palepale wa kuhakikisha madiwani
wanne wanabaki Kinondoni na kwamba hakuna mwenye mamlaka ya kuengua
mjumbe isipokuwa kifo na mahakama.
“Ubungo
hakuna tatizo. Ingawa maelezo yanafanana ya wajumbe watatu kutakiwa
kulingana na idadi ya madiwani wa kuchaguliwa. Ishu ipo Kinondoni kwa
sababu madiwani wetu wa viti maalumu wengi walikubaliwa,” alisema Kilewo.
Kuhusu
umeya baada ya manispaa hizo kugawanywa, Kilewo alisema jina la Mustafa
Muro, Diwani wa Kinondoni, ndilo lililopendekezwa na kupelekwa kwa
ajili ya kugombea umeya wa Kinondoni huku Boniface Jacob akiteuliwa
kugombea Ubungo.
Wakati
Kilewo akisema hayo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Salum
Madenge alisema mchakato wa kuwapata wagombea wa nafasi ya umeya na
naibu meya katika manispaa hizo ulitarajiwa kukamilika jana jioni.
“Mchakato
huu ulianza muda mrefu lakini leo (jana), jioni ndiyo kilele chake.
Wagombea watakaopatikana ni mahiri na CCM ipo fiti tunasubiri mechi
uwanjani,” alisema Madenge.
Kwa
nyakati tofauti, Manispaa za Kinondoni na Temeke zilifanya mgawanyo wa
madiwani baada ya Serikali kuzigawanya na kuunda halmashauri za Ubungo
na Kigamboni.
No comments