PAPA FRANCIS ASIHI USITISHWAJI VITA SYRIA MARA MOJA
Ndege za
kivita za Urusi zimerejelea mashambulizi mazito ya angani katika ngome
ya waasi Aleppo na kuua watu 25, miongoni mwao watoto 5. Papa Francis
ataka usitishwaji vita ili raia na watoto waondolewe.
Kiongozi
mkuu wa Kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis ameyasihi makundi
yanayopigana nchini Syria kusitisha vita mara moja. Wito wa Papa unajiri
kufuatia mashambulizi makali yanayofanywa na Urusi hivi sasa mjini
Aleppo ambapo watu 25 wameuawa wakiwemo watoto 5.
Mashambulizi
mazito ya angani ambayo yamefanywa na Urusi katika ngome za waasi
katika maeneo ya Aleppo ndiyo ya karibuni zaidi baada ya siku kadhaa za
utulivu kufuatia tangazo la Syria wiki jana kuwa ingelipunguza
mashambulizi, ili kuruhusu raia waondoke katika ngome za waasi.
Kulingana na kundi moja la kutetea haki za kibinadamu, watu 25 wameuawa
miongoni mwao watoto watano. Lakini maafisa wanaotoa misaada ya waokozi
wamesema zaidi ya watu 50 wameuawa kufuatia mashambulizi hayo ambayo
yamefanywa na ndege za Urusi.
Kiongozi
mkuu wa kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis ameyasihi makundi
yanayoshiriki vita nchini Syria kusitisha vita mara moja ili kuruhusu
raia waondolewe. Akiwahutubia maelfu ya watu katika uwanja wa Mtakatifu
Petero mjini Roma, Papa Francis amesema anatoa wito kwa viongozi
kunusuru raia hasa watoto ambao wamezingiriwa katika maeneo
yanayoshambiliwa. Papa Francis amesema
"Ninataka
kuangazia na nisisitize ukaribu wangu na waathiriwa wa mashambulizi ya
kinyama nchini Syria. Ni kwa haja ya dharura ambapo ninarejelea wito
wangu kwa nguvu zangu zote kuwasihi wanaohusika kuyasitisha mashambulizi
mara moja, ili kuruhusu raia waondolewe hasa watoto ambao bado
wamezingirwa katika maeneo yanayoshambuliwa".
Mashambulizi
hayo yanajiri wakati jamii ya kimataifa ikikumbwa na ghadhabu kuhusu
mustakabali wa raia 250,000 ambao bado wapo katika ngome za waasi.
Mashambulizi ambayo yanajiri baada ya kuvunjika kwa mkataba wa
usitishwaji vita ulioafikiwa kati ya Moscow na Washington. Suala ambalo
limezua mvutano kati ya Urusi na Ufaransa na mataifa mengine huku
Marekani ikitangaza kusitisha ushirikiano wake na Urusi kuhusu masuala
ya kusitisha vita Syria, nayo Ufaransa ikisema itataka Mahakama ya
kimataifa kuichunguza Urusi kwa makosa ya uhalifu wa kivita. Rais wa
Urusi Vladimir Putin amekatisha ziara yake iliyotarajiwa wiki kesho
mjini Paris baada ya rais wa Ufaransa Francois Hollande kusema
atazungumza naye tu kuhusu masuala ya Syria.
Naye
waziri wa masuala ya kigeni wa Uingereza Boris Johnson ameyataka makundi
ya kuteta haki za kibinadamu nchini mwake kupiga kambi nje ya afisi za
ubalozi wa Urusi kama njia ya kuishinikiza Urusi kukomesha mashambulizi
mjini Aleppo.
No comments