CUF TANGA WAMGOMEA PROFESA LIPUMBA
CHAMA
cha Wananchi (CUF) wilayani hapa kimetoa tamko la kutomtambua
Mwenyekiti wa Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, na kwamba hakitampokea
katika ziara yake.
Lipumba
anatarajia kuanza ziara mkoani Tanga kesho huku uongozi wa chama hicho
ukisisitiza kutambua uamuzi wa Mkutano Mkuu uliomwondoa madarakani na
wa Baraza Kuu kumvua uanachama.
Mwenyekiti
wa CUF wa Wilaya ya Tanga, Rashid Jumbe alitoa tamko hilo jana akieleza
kuwa hawatakuwa tayari kukaidi Katiba ya Chama chao na kwamba
hawatampokea na hakuna maandalizi yatakayofanyika kumpokea.
"Tumeambiwa
Lipumba ana dhamira ya kufanya ziara mkoani hapa. Sisi kwa uamuzi wa
Baraza hatumtambui, wala hatujaandaa maandalizi ya kumpokea.
“Wilaya
za Korogwe na Muheza ndizo zimesema atazitembelea, lakini sisi hatuko
pamoja nao na watakaompokea wataingia kwenye mgogoro mwingine kwa sababu
hatambuliki," alisema Jumbe.
Mwenyekiti
huyo pia alizungumzia mgogoro baina yao na CCM kutokana na sakata la
umeya ambapo alisema hatima ya mgogoro huo itajulikana baada ya mkutano
mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29.
Alisema
kutokana na sakata hilo walitoa malalamiko kwa viongozi mbalimbali
lakini hakuna hatua zozote zinazoendelea, hivyo Kamati ya Utendaji
iliwataka madiwani wa chama hicho kutohudhuria kikao chochote cha
Halmashauri hadi itakapotoa uamuzi.
"Tumetoa
malalamiko yetu kwa viongozi wa CCMna lengo letu ilikuwa tuonane na
Rais lakini tulimpata Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa aliyetwambia kuwa
atalifanyia kazi, lakini sasa tumeamua kupeleka malalamiko yetu kwa
wenye chama na wao ndio watakaotoa uamuzi juu ya mgogoro huo.
“Hivyo tumeitisha mkutano ambao utakuwa na wajumbe 440 ambapo tuna imani kuwa tatizo letu litakwisha Oktoba 29,” alisema Jumbe.
No comments