TRL KUONGEZA MABEHEWA 4 YA ABIRIA, TRENI YA KUTOKA DAR HADI PUGU
Na Frank Wandiba
KAMPUNI ya Reli Tanzania (TRL)
inakusudia kuongeza mabehewa 4 kwa ajili ya abiria wanaotumia huduma ya
usafiri wa treni kutoka kituo cha Dar es salaam hadi Pugu kufikia
mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu.
Ongezeko hilo litafanya mabehewa
kufikia 20 kutoka 16 yaliyopo sasa hali itakayoongeza ufanisi wa
utoaji wa huduma ya usafiri huo kwa abiria wanaotumia usafiri huo.
Hayo yamesemwa na Afisa Uhusiano
wa TRL, Midladjy Maez ambaye alisema hatua hiyo ni mkakati wa TRL wa
kukabiliana na changamoto ya usafiri huo kwa nyakati za asubuhi na jioni
ambapo choombo hicho cha usafiri kimekuwa kikikabiliwa na ongezeko
kubwa la watumiaji.
Maez alisema usafiri huo kwa
sasa umekuwa ukitumiwa na idadi kubwa ya wananchi hususani kwa nyakati
za asubuhi na jioni na hivyo kusababisha kuzidiwa na wasafiri
ikilinganisha na uwezo wa chombo hicho.
“Nawaomba abiria wote wafuate
taratibu wakati wa kutumia usafiri wetu ikiwemo kukata tiketi katika
vituo vyetu, kwani iwapo itabainika abairia hana tiketi na akaingia
ndani ya treni basi adhabu kali zitachuliwa dhidi yake ikiwemo kifungo
cha miezi 3 hadi 6” alisema Maez.
Aidha Maez aliwataka abiria
kutumia lugha za kistaarabu kwa wafanykazi wa treni pindi wanapobaini
changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza wakati wa kutumia vyombo
hivyo badala ya kutumia lugha zisizo za ustaarabu ambazo huwakwaza
watumishi wa treni hiyo.
Akizungumzia kuhusu mabadiliko
ya matumizi ya kituo cha Kamata kilichopo katika eneo la karikoo Jijini
Dar es Salaam, Maez aliwataka abiria wanaotumia kituo hicho kuhamia
katika kituo kidogo kilichopo ndani ya ofisi za TRL Mtaa wa Nkhurumah
ambapo abiria wote watahudumiwa pasipo na usumbufu.
Akifafanua zaidi Maez alisema ni
wajibu wa abiria wote kufuata sheria, kanuni na taratibu za matumizi ya
chombo hicho ikiwemo kukata tiketi kwani utaratibu huo hutumika
ulimwenguni kote na si Tanzania pekee.
No comments