MSAJILI MKUU WA MAHAKAMA TANZANIA AWATAKA MAHAKIMU KUZINGATIA SHERIA
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Katrina Revocati
amewataka mahakimu nchini kuzingatia sheria katika utendaji wao wa kazi hasa
katika utoaji wa dhamana.
Kauli ya Msajili imekuja wakati kukiwa na malalamiko dhidi
ya baadhi ya mahakimu kuwanyima dhamana washtakiwa ilhali mashtaka yao
yanaruhusu.
Aidha, kauli ya msajili huyo mkuu imekuja wakati mawakili wa
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema wakipambana ili mteja wao apate dhamana
baada ya kukwaa kisiki katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.
Mashtaka ambayo kwa mujibu wa sheria dhamana zake zimezuiwa
ni ya mauaji ya kukusudia, uhaini, utakatishaji wa fedha, wizi wa kutumia
silaha, usafirishaji binadamu na dawa za kulevya.
Hata hivyo, Mahakama inaweza kuzuia dhamana endapo kutakuwa
na pingamizi la kisheria, na mara nyingi mapingamizi hayo yamekuwa yakiambatana
na hati kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Msajili huyo alitoa maagizo hayo jana mjini Moshi alipokuwa
akizungumza na mahakimu wa ngazi zote katika mahakama za mjini Moshi baada ya
kumaliza ziara ya kikazi katika mkoa wa Kilimanjaro.
Taarifa iliyotolewa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda
ya Moshi, Bernard Mpepo ilisema msajili huyo waliwataka mahakimu watunze
maadili yao ili kujenga imani kwa jamii.
Msajili mkuu pia alitembelea Gereza Kuu la Karanga mjini
Moshi na kufanya ukaguzi wa kawaida na kisha kuzungumza na wafungwa, mahabusi
na wafanyakazi wa gereza.
Akiwa katika gereza hilo, msajili mkuu alisema mkakati wa
Mahakama ni kuona wateja wanapata huduma bora na ya haraka na tayari mahakimu
wamepewa malengo ya kumaliza kesi haraka.
Ili kuboresha huduma, alisema mwaka 2017 wamekubaliana
katika mahakama ya mwanzo, shauri lolote lisikae zaidi ya miezi sita wakati
mahakama ya wilaya na mkoa shauri lisikae zaidi ya miezi 12.
Pia mahakama imeingia mkataba na Shirika la Posta kusambaza
nakala za hukumu kwa wateja na nakala ya hukumu itakuwa inamfikia mdau ndani ya
siku 21.
Chini ya mkakati huo, nakala ya mwenendo wa shauri utamfikia
mteja wa mahakama ndani ya siku 21.
No comments