RAIS SAMIA MGENI RASMI TUZO ZA SAMIA KALAMU AWARDS
Na Neema Mpaka - Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya utoaji wa tuzo za waandishi wa habari za maendeleo zinazaofahamika kama SAMIA KALAMU AWARDS.
Hayo yamesemwa leo April 15,2015 jijini dare es salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Dokta Rose Reuben wakati akizungumza na waandishi.
Amesema tuzo hizo zimelenga kuhamasisha muandishi wa habari za maendeleo kujikita katika kufanya uchambuzi na utafiti wa kina,kuongeza maudhui ya ndani, kuzingatia weledi,maadili na uwajibikaji wa kitaaluma kukuza uzalendo na kujenga taswira chanya ya nchi.
Aidha amesema tuzo hizo za Samia Kalamu Award zinatokana na mafunzo yaliyotolewa mwaka jana 2024 kwa lengo la kukuza na kuendeleza uandishi wa habari za maendeleo nchini.
"Walengwa wa tuzo hizo ni waandishi wa habari, wachapishaji wa maudhui ya mitandaoni, maafisa habari, watangazaji na vyombo vya habari ambao walishiriki kwa kutuma kazi zilizorushwa ama kuchapishwa kupitia vyombo vyao". Alisema Dkt. Reuben
Kadhalika amesema tuzo hizo zimegawanyika katika makundi makuu matatu, kundi la kwanza linahusisha tuzo maalumu za kimataifa ambazo ni pamoja na tuzo ya chombo Cha habari mahiri kitaifa, Tuzo ya wanahabari wabobevu, Tuzo ya Afisa habari mahiri wa serikali, Tuzo ya mwandishi wa habari mahiri kitaifa na tuzo ya uandishi wa habari za matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Kundi la pili linajumuisha tuzo kwa vyombo vya habari vya Televisheni, vyombo vya habari mtandaoni, Redio ya kitaifa, Magazeti na Redio za kijamii.
Kundi la tatu ni tuzo za kisekta zitakazotolewa kwa waandishi wa habari waliobobea katika kuandika makala za maendeleo kwenye sekta mbalimbali ikiwemo afya, maji, nishati, mazingira, jinsia, wanawake na makundi maalumu, ujenzi, viwanda na biashara, maliasili na utalii, mifugo na uvuvi, uchumi wa buluu, kilimo, utamaduni, sanaa na michezo, TEHAMA na ubunifu, mazingira, ardhi na makazi, madini, fedha na uchumi, vijana, elimu na uwekezaji.
Aidha tukio la tuzo hizo litarushwa mubashara kupitia vituo mbalimbali vya Televisheni, Redio, na mitandao ya kijamii ili kuwawezesha wananchi wote waliowapigia kura waandishi na vyombo vya habari kufuatilia matokeo na utoaji tuzo.
Kadhalika washindi watatunukiwa zawadi mbele ya mgeni rasmi kama ishara ya kuthamini na kutambua mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika ustawi wa taifa.
Aidha amesema kuwa washiriki wanaotarajiwa kupata tuzo hizo ni washiriki 79.
Sambamba na hilo TAMWA na TCRA wanatoa wito kwa waandishi na vyombo vyote vya habari nchini kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha hafla hiyo ya kihistoria ambayo inatoa nafasi kwa wanahabari kutangaza mchango wao kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Tuzo hizo zilizoandaliwa na Chama Cha waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinatarajiwa kufanyika Aprili 29, 2025 katika ukumbi wa mabele, mabeyo complex jijini Dodoma.
Post Comment