ACT YAPINGA KAULI YA UKUAJI WA DEMOKRASIA NCHINI
Dar es salaam - Chama Cha ACT Wazalendo kimepinga kauli ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyoitoa bungeni wakati akisoma Bajeti ya ofisi yake na kueleza kuwa hali ya demokrasia hivi sasa nchini imeimarika.
Kauli hiyo imepingwa na Waziri Mkuu Kivuli wa ACT, Isihaka Mchinjita wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Aprili 10, 2025, alipokuwa akifanya uchambuzi wa bajeti ya ofisi hiyo.
Akizungumzia hilo Mchinjita alisema kwamba kuna mambo ambayo yamekuwa yakifanyika yamedhihirisha wazi kwamba suala la demokrasia bado halijaimarika.
Akielezea mambo hayo alisema, "Takribani chaguzi tatu zilizopita tumeshuhudia wagombea wa vyama vya upinzani wakienguliwa, tumeshuhudia uwepo wa kura feki mitaani na vyombo vya usalama vikitumika kuibeba CCM.
Aliongeza kuwa,"Hali ya demokrasia nchini ni mbaya mno! kwa hivyo sisi ACT Wazalendo tumeamua kutoa uongozi katika kudai mabadiliko mahususi ya mifumo ya uchaguzi, tumeamua kupigania kurejesha heshima ya kura.
"Sisi ACT Wazalendo, tunataka Makamishna wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi wapatikane kwa ushindani na Wakurugenzi wa Halmashauri wasiwe wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo."
Post Comment