Breaking News

RITA KUWANOA WAJUMBE WA BODI, TAASISI ZA WADHAMINI

Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA Bw Frank Kanyusi akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafunzo maalum yaliyoandaliwa na Taasisi yake kwaajili ya wajumbe wa Bodi,Taasisi ambazo zimesajiliwa Dar es salaam yatakayofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Jijini kesho

Na Mwandishi Wetu - Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) umeandaa mafunzo/mkutano maalum kwa Wajumbe wote wa Bodi za Wadhamini wa Taasisi zilizosajiliwa RITA zilizopo Dar es Salaam yakayofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Kumbumbuku ya Mwalimu Nyerere Jijini kesho yakilenga kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Hayo yamesemwa na Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi ambaye aliwataka wajumbe wote kukamilisha kujisajili kwa ajili ya kushiriki kwenye mafunzo hayo Maalum yaliyondaliwa na taasisi yake ambapo Waziri wa Sheria na Katiba, Dkt Damas Ndumbaro anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

“Wadhamini watakaoshiriki mafunzo hayo maalum watatakiwa kujisajili kupitia kiunganishi kifuatacho https:tsms.gov.go.tz/login na watakaoshiriki watapata fursa ya kupata miongozo ya jinsi ya kupata huduma mbalimbali ikiwa pamoja na kufanya marejesho kwa mfumo wa kidijitali wa eRITA,” amesema Kanyusi.

Bodi za wdhamini ni pamoja na Vyama vya Siasa, Taasisi na Madhehebu ya kidini, Vyama/Vilabu vya michezo, Taasisi binafsi za kijamii zilizo na wanachama na zinazomiliki mali na Vyama vya Kiuchumi.

Kanyusi amesema kwa mujibu wa Sheria ya Muunganisho wa Wadhamini Sura ya 318 Toleo la 2002 ni mtu yeyote au wanachama wa Taasisi aliyepewa mamlaka au nafasi ya uaminifu ya kusimamia mali kwa faida ya wanachama/walengwa kisheria kwa malengo/madhumuni yaliyoainishwa.

“RITA ina matumaini kwamba baada ya mafunzo hayo, tunatarajia masuala ya ubadhirifu, matumizi mabaya ya Madaraka na migogoro itapungua au kuisha kabisa hivyo Taasisi hizo kuweza kufikia malengo ya kuanzishwa kwake.,” alisitiza.

Ameseman RITA imesajili taasisi zaidi ya 4,300 nchini kote ambapo zaidi ya asilimia 65 ya taasisi hizo zipo Dar es salaam na hivyo kuwataka wadhamini hao wajitokeza kwa wingi kuhudhuria mafunzo hayo muhimu kwa ustawi wa taasisi zao.

“Chimbuko la Mkutano huo ni matokea ya ziara ambazo Wakala umefanya kuzitembelea taasisi hizo na kubaini sehemu kubwa ya wadhamini hawana ufahamu wa kutosha wa majukumu na wajibu wao katika kusimamia mali za taasisi zao hivyo kushindwa kuzisimamia ipasavyo.,” amesema Kanyusi na kuongeza kuwa wapo wadhamini ambao kwa kujua au kutokujua wamekuwa wakikiuka misingi na Katiba za taasisi zao na kusababisha migogoro na ubadhirifu wa mali.

No comments