Breaking News

RAIS DKT. SAMIA APONGEZWA MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA

Na Mwandishi wetu, Arusha - Tanzania imetajwa kuwa Nchi inayopiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya kwa kuwekeza zaidi katika eneo la kinga kwa kujenga vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya kwa waraibu wa dawa hizo katika hospitali za Kanda na Rufaa pamoja na utoaji elimu kwa makundi mbalimbali ikiwemo klabu za vijana shuleni.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga Jijini Arusha wakati akifungua Mkutano wa siku nne wa Jukwaa la kimataifa lililo chini ya Umoja wa Afrika(AU) kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama Kuhusu Kuweka Nguvu za pamoja katika kupunguza uhitaji na usambazaji wa Dawa za kulevya katika Nchi wanachama za Umoja Wa Afrika.
Mhe. Nderiananga amesema lengo la mkutano huo ni kubadilishana uzoefu wa masuala ya Afya katika mapambano dhidi ya Dawa za kulevya akisema kuwa mafanikio hayo yametokana na kazi kubwa inayofanywa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uwekezaji kwenye sekta ya afya hususan ujenzi wa Vituo vya Tiba Saidizi kwa waathirika wa dawa za kulevya (MAT CLINICS) ambavyo husimamiwa na Serikali.

“Tumepiga hatua zaidi katika udhibiti wa dawa hizi nchini na wenzetu Nchi za Umoja wa Afrika kuungana kwa pamoja katika kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya , kudhibiti mbinu wanazotumia wauzaji na watumiaji wa dawa hizo na uimarishwaji wa maeneo ya mipakani kuzia uingizwaji wa dawa hizo nchini kwetu,"Amesema Mhe. Nderiananga.
Aidha Amebainisha kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya mitaani kwa kuhakikisha wanaokamatwa na dawa za kulevya wanachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.

“Jitihada za kudhibiti dawa hizi haziwezi kufanikiwa bila kushirikiana na Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika ambazo ni Nchi zote za Bara la Afrika zikiwemo Namibia, Botswana, Zambia, Nigeria, Kenya na Sierra Leone. Kwa Tanzania kwa sasa tumeanzisha Kituo cha Utoaji Huduma (Call Centre) ambapo mwananchi ana uwezo wa kupiga simu kutoa taarifa za uwepo wa dawa na kulevya au viashiria ili uchunguzi ufanyike na wahusike wachukulie hatua,”Ameeleza.
Naye Naibu Katibu Msaidizi, Mipango, Sera za Kimataifa anayeshughulikia Ofisi ya Afrika na Mashariki ya Kati katika Masuala ya Kimataifa ya Utekelezaji wa Sheria,(INL) Bi. Maggie Nadri amesema vifo vinavyotokana na matumizi ya dawa za kulevya yaliyopitiliza vimepungua kwa asilimia 12 katika nchi za Umoja wa Afrika.

“Kama Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika ni wakati sasa wa kuongeza nguvu eneo la utoaji elimu kwa vijana shuleni, vyuoni ili kupunguza matumizi ya dawa hizi kwa kuwajengea uwezo wataalam wa afya na Mamlaka za ulinzi kubadilishana mbinu za kudhibiti matumizi ya dawa hizo katika maeneo ya mipakani, majini, ardhini na kwingineko ili kuwezesha wananchi wengi kutojiingiza katika dawa za kulevya ambazo zimekuwa zikiathiri nguvu kazi ya Nchi zetu,” Amesisitiza Bi. Maggie.



No comments