Breaking News

MRADI WA UJENZI BOMBA LA MAFUTA GHAFI (EACOP) KUIMARISHA MAHUSIANO KATI YA TANZANIA NA UGANDA BALOZI - MWESIGYE

Tanga - Balozi wa Uganda nchini, Mhe Kanali mstaafu Fred Mwesigye, amesema Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima nchini humo hadi Chongoleani, Tanga, unapaswa kuibua na kuendeleza miradi inayoimarisha mahusiano na hifadhi ya mazingira na utamaduni kati ya nchi mbili hizo.

Mhe Balozi Kanali mstaafu Mwesigye, ameyasema hayo leo Desemba 10, 2024, alipomtembelea Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dk Batilda Burian ofisini kwake, akiwa katika ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali yanayopitiwa na EACOP.

Amesema mradi huo unaohusisha maslahi ya Uganda na Tanzania, haupaswi kufikia ukomo wake kwenye manufaa ya kiuchumi pekee, bali kuziunganisha jamii hasa za Hoima na Tanga, kushiriki programu za hifadhi ya mazingira na tamaduni zilizopo kwenye maeneo hayo.

Kwa mujibu wa Mhe Balozi Kanali mstaafu Mwesigye, hatua hizo zikitekelezwa kwa kizazi cha sasa na baadaye, zitaimarisha zaidi ushirikiano uliodumu kwa muda mrefu kati ya Uganda na Tanzania.

Mhe Balozi Kanali mstaafu Mwesigye amesema kutokana na dhana hiyo, ipo haja ya kuzifanya Tanga na Hoima kuwa ‘miji pacha’ ambayo watu wake hususani vijana, watatembeleana na kushirikiana katika nyanja za kijamii, uchumi, utamaduni na mazingira, ikiwemo kupanda miti ili kuingia kwenye biashara ya hewa ya ukaa.
Kwa upande wake, Mhe Balozi Dk Batilda, amempongeza Mhe Balozi Kanali mstaafu Mwesigye kwa ziara na mawazo chanya, yanayolenga kukuza ushirikiano mwema katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Mhe Balozi Dk Batilda amesema, uongozi wa mkoa wa Tanga umeshabuni matukio kadhaa ya kijamii yaliyo wazi kwa raia wa Uganda kushiriki, ikiwemo mbio za kimataifa za Chongoleani Marathon na tamasha la utamaduni na malikale za Tanga.

Pia, Mhe Balozi Dk Batilda amesema, fursa nyingine zinazoweza kufanyika ni maonesho ya barabarani maarufu kama road show, na kuanzisha mpango wa kubadilishana uzoefu kwa wakazi wa Tanga na Hoima.


No comments