Breaking News

SERA YA CHAKULA NA LISHE KUKAMILISHWA ILI KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA UDUMAVU

Na WAF - DODOMA 
Wizara ya afya inaendelea kukamilisha Sera ya chakula na lishe ili kukabiliana na changamoto ya utapiamlo na udumavu nchini kwa kujumuisha mapendekezo yaliyotolewa kwenye mkutano wa tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe nchini. 

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Agosti 31, 2024 wakati akimkaribisha Mgeni rasmi ambae ni Waziri wa Nchi ofisi ya Rais - TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa kwenye mkutano wa Nane wa Tathmini ya Mkataba wa Lishe na kutambulisha mpango wa Taifa wa uwekezaji katika Afya ya Mama na Mtoto uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi za Wizara ya Afya uliopo katika Mji wa Kiserikali (Mtumba) mkoani Dodoma.

“Tutaendelea kukamilisha Sera ya Taifa ya Chakula na Lishe ili iweze kutusaidia kutuongoza kukabiliana na changamoto mbalimbali za lishe na kwa kushirikiana na wadau kama Shirika la SANKU tumezindua kiwanda cha kuzalisha virutubishi nchini ili kurahisisha upatikanaji wa virutubishi nchini na unga utakaotumika na watoto wa mashuleni hapa nchini ni lazima uwe umeongezwa virutubishi.”Amesema Waziri Mhagama.
Waziri Mhagama amesema katika kuhakikisha kwamba kuna muendelezo wa shughuli zilizokuwa zinafanywa na Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Wizara imekamilisha maandalizi ya kuanzishwa kwa programu maalum ya lishe ambayo itachukua jukumu la TFNC.

Waziri Jenista pia amegusia suala la ubora wa mifumo ya kusajili mgonjwa pindi afikapo katika vituo vya kutolea huduma za afya na mfumo huo uwezeshe kuweka miadi na kupata huduma kwa wakati. 

“Kazi kubwa ambayo ipo mbele yetu ni kuwa na mifumo imara ya kusimamia sekta ya afya ikiunganishwa na swala zima la lishe ili tuwe na matokeo chanya, tunatamani huduma za afya zinazotolewa kwenye Afya Msingi ziunganishwe moja kwa moja kwenye maeneo ya hospitali ya wilaya, Rufaa za mikoa, hospitali za kanda, hata hospitali kuu kwakua eneo hili la mifumo ni eneo kuu na sisi tunalipa kipaumbele, mifumo nayo izungumze ili tuweze kusomana na kuwasiliana”. Amesema Waziri Mhagama

Katika kutekeleza Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ikiwa ni moja ya hatua muhimu kuelekea kuwa na Afya kwa Wote Waziri Mhagama ametoa rai kwa Wakuu wa Mikoa na Viongozi wote kufanya uhamasishaji ili wananchi waweze kuelewa na kujiunga ili kuwa na uhakika wa matibabu katika kipindi chote na kunufaika na uwekezaji Mkubwa uliofanywa na Rais Dkt. Samia katika sekta ya afya kwa nyanja zote.

Awali akiwasilsha Mada Mkurugenzi wa Idara ya Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Ntuli Kapologwe amebaiinisha hali ya ugonjwa wa MPOX nchini amabo amesema hadi sasa Tanzania bado haina mgonjwa huo.

No comments