Breaking News

ACT WAZALENDO YALAANI VITENDO VYA UKIUKWAJI WA HAKI ZA WANANCHI WA KALIUA

Chama cha ACT WAZALENDO kimelaani ukiukwaji Mkubwa wa Haki za Binadamu dhidi ya Wananchi katika vijiji 11 vya Kaliua Mkoani Tabora na kulitaka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunda kamati ya kuchunguza vitendo hivyo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Agost 30, 2024 makao makuu ya chama hicho Jijini Dar es Salaam Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Mbarala Maharagande  amesema kumekuwepo na oparesheni za kuwaondoa wananchi zilizofanywa Agosti 2021 katika vijiji 11 vya Usinge, Luganjo, Wachawaseme, Igagala Na.3, Igagala Na 4, Igagala Na 7, Igagala Na 9, Kombe, Tuombe Mungu na Limbu la Siasa. 

Na kurudiwa tena hivikaribuni Agosti 8, 2024 katika vijiji vya Chawasema, Luganjo na Kombe zimesababishaathari kubwa kama vile vifo vya watu 12, vipigo, kujeruhiwa, kuchomwa na kubomolewanyumba, shule na kuporwamifugo, vyakula, vyombo vya usafiri na samani za nyumbani.

“Serikali kupitia TAWA, TFS na Mkuu wa Wilaya wa Kaliua kutwaa eneo la hifadhi ya Ardhi ya vijiji 11 na kubadilisha kuwa Pori la Akiba la Igombe bila ridhaa yao Mwaka 2007 vijiji 11 vilikubaliana kutenga sehemu za ardhi zao za vijiji eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,800 kwa ajili ya kuanzisha jumuiya ya hifadhi ya wanyama iliyojulikana kwa jina la ISAWIMA (Igombe and Sagara Wildlife Management Area), Lakini cha kusikitisha hata lile eneo dogo walilobakiwa nalo wananchi sasa wanapokonywa kwa kushushiwa vipigo,kubakwa na wengine kuuawa kwa risasi za moto”. Alisema Maharagande.

Alisema chama kinatoa wito kwa Serikali kusitisha mara moja operesheni hizo za kuwaondoa wananchi katika vijiji vya Chawasema, Lugano na Kombe kwa kuwa operesheni hiyo zinakiuka sheria ya ardhi ya vijiji ya mwaka 1999, nakubainisha  kuwa madai ya Serikali kuwa wananchi hao wamevamia hifadhi ni propaganda.

Pia chama kimetoa wito kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan  kuunda kamati ya kupitia maeneo yote yenye migogoro ya mipaka kati ya vijiji na mamlaka za hifadhi nchini pamoja na Serikali kuwalipa fidia wananchi wote walioathiriwa na operesheni ya kuwaondoa wananchi wa vijiji 11 vya ISAWIMA

Katika hatua nyingine Maharagande  amemtaka Mkuu wa wilaya ya Kaliua na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, watendaji, Maafisa pamoja  na watumishi wa TAWA) na TFS wanapaswa kuchukuliwa hatua kwa kuruhusu vikosi vya Ulinzi vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wanamgambo na askari wa TFS kufanya uonevu kwa wananchi hao. 

No comments