Breaking News

WAZIRI KAIRUKI: WADAU WA UFUGAJI NYUKI TUMIENI FURSA YA MKUTANO WA DUNIA WA UFUGAJI NYUKI 2027 KUVUTIA WAWEKEZAJI

Dar es salaam:
Wadau wa ufugaji nyuki nchini wametakiwa kutumia fursa ya mkutano wa Dunia wa Ufugaji Nyuki  (APIMONDIA)  utakaofanyika nchini 2027 kuvutia wawekezaji na kuongeza tija katika ufugaji na biashara nzima ya mazao ya nyuki na utalii.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) katika mkutano na vyombo vya habari uliofanyika  kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam .

"Tumieni mkutano huu vizuri kwa  kuongeza tija katika ufugaji na biashara nzima ya mazao ya nyuki, kuongeza wigo wa mashirikiano na taasisi mbalimbali duniani katika kuvutia uwekezaji katika sekta hiyo pamoja na  kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu shughuli za ufugaji nyuki hususani teknolojia na mbinu mbalimbali za kuboresha na kuendeleza sekta hii " Mhe. Kairuki amesisitiza. 

Ametoa wito kwa watanzania na wadau mbalimbali kuwekeza katika sekta hiyo kwa kuwa kwa sasa uzalishaji wa asali ni tani takribani elfu 32 tu wakati kama taifa kuna uwezo wa laki 138

Aidha, amesema mkakati wa Serikali kwa sasa ni ule ujulikanao kama "achia shoka kamata mzinga" ambao umelenga  kudhibiti ukataji wa miti ovyo na badala yake kujikita katika kuongeza mizinga.

Amesema Tanzania ni nchi ya 14 duniani na ya 2 Afrika katika uzalishaji wa asali.

Hata hivyo, amesema kuwa kwa Tanzania kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa APIMONDIA Tanzania inakwenda kuwa nchi ya pili Barani Afrika kupewa jukumu hilo kubwa la kuandaa kongresi hiyo tangu kuanzishwa kwa APIMONDIA miaka takribani 130 iliyopita. 

Kwa mara kwanza Kongresi hiyo  kufanyika Barani Afrika ilikuwa mwaka 2001 ilipofanyika nchini Afrika ya Kusini.

Amefafanua kuwa mkutano huo unakadiriwa kushirikisha wadau zaidi ya 6,000 toka mataifa mbalimbali dunia hivyo Tanzania kuwa mwenyeji wa kongresi hiyo kunatarajiwa kuleta manufaa makubwa ya kuchochea ukuaji wa sekta ya nyuki na uhifadhi, kuongeza mchango wa sekta katika pato la taifa, kuchochea utalii kwa ujumla nchini na kuvutia uwekezaji wa viwanda na teknolojia katika sekta ya ufugaji nyuki.

Ushindi huo ulitangazwa na Rais wa APIMONDIA, Ndugu Jeff Pettis mbele ya wajumbe waliohudhuria shughuli za kuhitimisha mkutano mkuu wa 48 wa Shirikisho hilo uliomalizika mwisho nchini Chile.

Ushindi huo ni hatua muhimu kwa Tanzania kama nchi lakini pia kwa Bara zima la Afrika  kwani unakwenda kuwakutanisha Wataalamu mbalimbali wakiwemo  wafugaji  nyuki duniani  wafanyabiashara, wasomi, watafiti pamoja na wachakataji wa mazao ya nyuki. 

APIMONDIA ni Shirikisho la Umoja wa Vyama vya Wafugaji nyuki Duniani lililoanzishwa mwaka 1895 nchini Italia huku. Tanzania ilijiunga katika shirikisho hilo mwaka 1984 ambapo  Tanzania kwa mwaka huu nchini Chile iliibuka  kuwa mshindi wa kinyanganyiro cha kuandaa Mkutano wa 50 mwaka 2027 ni Tanzania,



No comments