Breaking News

RAIS SAMIA KUFUNGUA MKUTANO WA KUJADILI RIPOTI YA KIKOSI KAZI, DEMOKRASIA NA HALI YA SIASA NCHINI

Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa nchini bwana Mohamed Ali Ahmed akifafanua jambo katika kikao na waandishi wa habari kuhusu mkutano wa wadau wa demokrasia unaotarajiwa kufanyika Septemba 11, 2023 na kufunguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan jijini Dar es salaam.

Na mwandishi wetu
Zaidi ya washiriki 500 kutoka taasisi za kisiasa, dini, asasi za kiraia na wengine watakutana kwa siku tatu jijini Dar es Salaam kupokea ripoti ya kikosi kazi na  kufanya tathmini ya demokrasia na hali ya kisiasa nchini.

Hayo yamesemwa na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, bwana Mohamed Ali Ahmed amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ndiye atafungua kikao hicho.

Amesema kikao hicho cha aina yake kitafanya tathmini ya utekelezaji wa ripoti ya kikosi kazi, demokrasia na hali ya siasa 

"Jumatatu Septemba 11 hadi 13, 2023 wadau wa vyama vya siasa, asasi za kidini, kiraia na wengine watajadiliana kuhusu tathmini ya utekelezaji wa ripoti ya kikosi kazi, demokrasia na hali ya kisasa, tunawaomba watu wote walioalikwa kujitokeza kwa wingi," amesema.

Ahmed amesema Rais Samia amekuwa akisisitiza 4R katika uongozi wake akimaanisha maridhiano, ustahimilivu, mabadiliko na kujenga upya, hivyo kupitia mkutano huo wadau watapata nafasi ya kujadiliana kwa kina na uhuru.

Naibu Msajili amesema mkutano huo ambao unatarajiwa kufungwa Septemba 13 na Rais wa Zanzibar Dkt Hussein Ali Mwinyi umebeba kauli mbiu inayosema imarisha demokrasia dumisha amani, hivyo ni imani yetu kubwa washiriki watazingatia hilo katika mijadala yao.

Amesema mkutano huo unatarajiwa kutoka na maazimio kuhusu utekelezaji wa ripoti ya kikosi kazi iwapo wataona utekelezaji haukufanyika. 

Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Maandalizi ya amesema mkutano huo ni mwendelezo wa ule wa Desemba 15 hadi 17, 2021 ambao ulifanyika mkoani Dodoma na kuzaa kikosi kazi ambacho kilipokea maoni ya wadau, ikiwemo mchakato wa kupatika kwa Katiba mpya. 

"Waswahili wanasema mwiba ulipoingilia ndipo unapotokea, hivyo tumewaita wadau ili wapate fursa ya kujadili kwa kina kuhusu mapendekezo yao," amesema.

Ripoti ya Kikosi Kazi:

Ripoti ya kikosi kazi ilitoa mapendekezo 19 ya kufanyiwa kazi ambapo moja wapo ni kuhusu mikutano ya hadadhara kuruhusiwa jambo ambalo Rais Samia aliridhia na vyama vya siasa vimeanza kutekeleza kwa vitendo.

Pia Kikosi Kazi kimependekeza Sheria ya Vyama vya Siasa ifanyiwe marekebisho ili, kulipatia Baraza la Vyama vya Siasa mamlaka ya kuishughulikia suala la uvunjifu wa maadili ya Vyama vya Siasa kupitia Kamati yake ya Maadili na Msajili wa Vyama vya Siasa awe na mamlaka ya kuandaa mwongozo wa uchaguzi wa ndani ya vyama .

“Kuweka masharti kwamba idadi ya jinsi moja katika vyombo vya maamuzi vya chama cha siasa isipungue asilimia 40; na kukitaka kila chama cha siasa kuwa na sera ya ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika shughuli za chama husika,” ilisema.

Eneo lingine ambalo Kikosi Kazi kimependekeza ni kuhusu ruzuku kwa vyama vya siasa  ambapo mfumo wa sasa wa kugawa ruzuku ya Serikali kwa vyama uendelee, isipokuwa asilimia 10 ya fedha za ruzuku kwa vyama vya siasa zilizotengwa katika bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha husika, igawiwe sawa kwa vyama vyote vya siasa vyenye usajili kamili kwa mujibu wa vigezo na masharti husika.

Pia Kikosi Kazi kimependekeza mfumo wa uchaguzi, kwa Mfumo Mseto wa Uchaguzi uendelee kutumika kwa uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani. 

Aidha, katika uchaguzi wa Rais ili mgombea ashinde uchaguzi iwe ni lazima apate zaidi ya asilimia hamsini ya kura zote halali zilizopigwa  na uchaguzi wa wabunge, madiwani na uchaguzi wa Serikali za Mitaa uendelee kutumia Mfumo wa Mshindi kwa Kura Nyingi; na Mfumo wa Uwiano wa kura uendelee kutumika kupata wabunge na madiwani wa viti maalum vya wanawake.

“Eneo la nne ni Uhuru wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi,  Uteuzi wa Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi, Matokeo ya Uchaguzi wa Rais wa Tanzania kutohojiwa Mahakamani,  Watendaji wa Tume ya Uchaguzi, Bajeti ya Tume ya Uchaguzi, Usimamizi wa Uchaguzi, Sheria Zinazosimamia Masuala ya Uchaguzi na matumizi ya TEHAMA katika uchaguzi

Kikosi Kazi hiyi kimependekeza ushiriki wa wanawake, vijana, watu wenye ulemavu katika siasa, demokrasia na uongozi na utoaji wa elimu ya uraia ikiwemo elimu ya mpiga kura nchini.

Eneo lingine ni kuhusu rushwa na maadili katika siasa na uchaguzi, mfumo wa maridhiano ili kudumisha haki, amani, utulivu na umoja wa kitaifa nchini, mawasiliano kwa umma, vyombo vya habari na siasa na Katiba Mpya ya Tanzania ambapo Kikosi Kazi kinapendekeza kukamilishwa kwa mchakato wa kupata Katiba Mpya kupitia hatua sita.

“Hatua ya kwanza mjadala wa kitaifa ili kupata muafaka katika masuala ya msingi kabla ya kuanza mchakato wa kuandika katiba mpya.

Mjadala huu ufanyike kwa ushiriki mpana wa wananchi. masuala ya msingi yanajumuisha muundo wa muungano, madaraka ya rais, mfumo wa uchaguzi, madaraka ya serikali za mitaa, rushwa na maadili na mengineyo yatakayojitokeza.

Hatua ya pili: kuhuisha sheria ya mabadiliko ya katiba na sheria ya kura ya maoni, yakiwemo kuainisha muda wa mchakato mzima, kutambua kuanzishwa kwa jopo la wataalam na kuainisha misingi ya kuzingatiwa katika mchakato wa mabadiliko ya katiba.

Aidha, kuwepo na ushirikishwaji mpana wa wananchi katika mchakato wa kuhuisha sheria hiyo, kwa kufuata taratibu za utungaji wa sheria nchini.

Hatua ya nyingine kuundwa kwa jopo la wataalam baada ya sheria ya mabadiliko ya katiba kuhuishwa na mengine mengi. 

No comments