Breaking News

EWURA YATOA ONYO KWA WAFANYABIASHARA WANAOKIUKA MASHARTI YA LESENI, YAFUNGIA VITUO VINGINE VITATU

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imevifungia vituo vingine vitatu kutofanya Biashara ya mafuta kwa miezi sita.

Akizungumza na waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Dkt. James Andilile amevitaja vituo hivyo kuwa ni Camel Oil- Gairo Petrol Station chenye Leseni Namba PRL-2019-164.

Vituo vingine ni Petcom-Mbalizi Petrol Station chenye Leseni Namba PRL-2023-025 na Rashal Petroleum Ltd-Mkalama chenye Leseni Namba PRL-2019-034.

“Pamoja na kuwepo na mafuta, baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakichukua mafuta na kuchelewesha kufikisha vituoni huku wengine wakiwa na mafuta kwenye visima lakini hawauzi, hivyo kusababisha kuwa na usumbufu mkubwa kwa wananchi. Kutokana na ufichaji mafuta, EWURA imevichukulia hatua vituo nane ambavyo vimejihusisha na tabia ya kuficha mafuta,” amesema Dkt. Andilile na kuongeza,

“Hata hivyo, EWURA ilikuwa ikivichunguza vituo vingine sita vilivyoonesha kutofanya Biashara ya mafuta kwa sababu mbalimbali ambapo uchunguzi umebaini kuwa vituo vitatu Kati ya hivyo vimebainika kutouza mafuta kwa maslahi binafsi,”.

Dkt. Andilile ameeleza kwamba kufungiwa kwa vituo hivyo kwa miezi sita kunafanya vituo vilivyofungiwa kuwa vitano ambapo vituo vitatu bado vinachunguzwa kwa ajili ya hatua zaidi.

Ametumia fursa hiyo kutoa onyo kwa wafanyabiashara ya mafuta, Wenye vituo na maghara ya mafuta kufuata masharti ya Leseni zao ya kutoa huduma.

Kwamba watakapothibitika kukikuka masharti ya Leseni EWURA haitasita kuwachukulia hatua ikiwemo kuwafungia kutoa huduma.

Dkt. Andilile amewatoa hofu wananchi kwamba hatua hizo zinazochukuliwa hazina nia ya kumuonea mtu bali ni kwa mujibu wa sheria ambapo amebainisha kuwa wafanyabiashara watakaoona wameonewa wakate rufaa.

No comments