Breaking News

MAHIMBALI ATOA WITO KWA WACHIMBAJI WADOGO KUITUMIA WIZARA

Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri  Mahimbali amewataka Wachimbaji  Wadogo kupitia Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA) kushirikiana na Wizara hiyo katika shughuli  za uchimbaji ili kuweza kuinua sekta ya uchimbaji mdogo nchini.

Amesema  ushirikiano  mzuri baina ya wachimbaji  na Wizara utaiwezesha Sekta ya Madini kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa.

Aidha, Mahimbali amesema wakati Wizara inajizatiti kuweka na kusimamia Mikakati  na Sera zenye nguvu ili kuimarisha sekta ya uchimbaji mdogo  ni wajibu wa wachimbaji kuchimba kwa weledi ili kuongeza mapato na kulipa kodi na maduhuli.

Amewataka kuwa wawazi katika kutatua kero na changamoto  ili kuiwezesha Serikali kuondoa vikwazo katika uchimbaji kwa urahisi na kuahidi kuendelea kutatua changamoto  zinazowasilishwa Wizarani kwa uharaka.

Naye, Kamishna wa Madini Dkt. AbdulRahman Mwanga  amewataka wachimbaji wa madini kutambua namna Wizara inavyowathamini na kufungua milango ili kuweza kutatua kero na kuleta maendeleo  kupitia sekta hiyo.

Kwa upande  wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambalo ni mlezi  wa wachimbaji wadogo,   amesema  FEMATA inapaswa kujua kwamba Serikali  ina msukumo  mkubwa katika  kuwasaidia  wachimbaji wadogo  ni wajibu wao kuhakikisha  wanatoa ushirikiano  kwa Wizara.

Amepongeza jitihada za Shirikisho  hilo kwa kuonesha nia ya dhati ya kutaka kuendelea na kukuza uchumi wa Serikali  kupitia sekta ya wachimbaji  wadogo  ambao wengi wao ni wazawa. 

Amesema Sekta ya Madini inawagusa watanzania na kwamba kuendeleza wachimbaji  wadogo  ni kuendeleza maisha ya watanzania  wanaotegemea sekta hiyo.

Akitoa shukrani kwa Wizara, Makamu Mwenyekiti wa FEMATA  Alfred Luvanda amesema hafla hiyo imekuwa na tija sana katika sekta ya wachimbaji  wadogo. 

"Ni nafasi adhimu kuona watendaji  wakuu wa Wizara  wanatenga muda kukutana na wachimbaji  moja kwa moja, hali hii inaamsha imani ya wachimbaji  kwa Serikali," amesema  Luvanda.

Ameiomba Wizara isaidie kuwaunganisha  wachimbaji  wadogo wote ili waweze kufanya kazi chini ya mwamvuli moja ili kuimarisha sekta hiyo.

Ameipongeza STAMICO kwa kuendelea kuwasimamia vizuri wachimbaji  wadogo  licha ya majukumu makubwa waliyonayo.







No comments