Wahadzabe Waiomba Serikali Iwapatie Tani 2 Za Bangi
Jamii ya Wahadzabe wanaojishughulisha na
uwindaji, kurina asali na kukusanya matunda porini, wameomba kupelekewa msaada
wa bangi angalau tani mbili watakayoitumia kwa mwaka mmoja.
Wahadzabe wanaokadiriwa kufikia 500 ni jamii
inayoishi porini maeneo ya Endamaghan, Kandeni Tarafa ya Eyasi Wilaya ya Karatu
mkoani Arusha.
Jamii hiyo, bado inakabiliwa na umasikini
licha ya kuwa kivutio cha watalii katika Ziwa Eyasi.
Ombi hilo walilitoa juzi katika Kijiji cha
Endamaghan, wakati walipotembelewa na timu ya wataalamu kutoka serikalini
iliyoteuliwa kuandaa mapendekezo ya muundo wa kipindi cha pili cha mpango wa
kunusuru kaya masikini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Akizungumza na Gazeti la Mtanzania
katika eneo la makazi yao yenye nyumba za asili za nyasi zilizoonekana kuwa
wazi kutokana na kufunikiwa na nyasi kidogo, Mwenyekiti wa jamii hiyo, Julius
Ndaya alizitaja sababu alizodai ni za msingi za kuomba wapelekewe bangi.
Alisema shughuli za kutembea kutafuta wanyama
kwa ajili ya kitoweo huwalazimisha kutembea umbali mrefu kiasi cha kilomita 50,
kazi ambayo huwa ni sehemu ya majukumu ya mwanamume katika jamii hiyo.
“Kiasi hiki cha tani mbili kinaweza kututosha
watu kama 100 au 200 kwa miezi 6, tunavuta bangi si kama ambavyo wengine
au Serikali wanafikiria kwamba tunaweza kusababisha vurugu, kuvunja nyumba za
watu, kuiba wala kugombana na jamii nyingine, hapana.
“Mmea huu tumeukuta babu zetu wakiwa
wanauvuta wameturithisha, tunaendelea kuvuta bila kuwa na madhara yoyote. Hii
ni sehemu ya kiburudisho kwetu, huku porini hatunywi pombe hii ndio pombe yetu.
“Ikiwezekana turuhusiwe kulima angalau bustani za bangi lakini changamoto kubwa
tunayokutana nayo ni pale Serikali inapopiga marufuku zao hili kwa madai kuwa
ni sehemu ya dawa za kulevya,” alisema Ndaya.
Kiongozi wa jamii hiyo alikwenda mbali na
kueleza pindi wanapovuta bangi huchangamsha akili na miili yao, hivyo hujikuta
wakipiga hadithi za matukio ya uwindaji porini au namna walivyokabiliana na au
kukurupushana na wanyama wakati wa uwindaji.
Katika eneo la jamii hiyo lenye nyumba za
asili za nyasi zikiwa zimezungukwa na mafuvu ya wanyama pori na miti mikubwa,
lilikuwa na wanawake watu wazima walionekana wamekaa kwenye makundi pamoja na
vijana wa kiume wakiendelea kuvuta bangi.
Akifafanua kuhusu maombi ya Wahadzabe kuomba
tani mbili za bangi, Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Theresia Mahongo alisema
Serikali haiwezi kukubaliana na maombi hayo.
“Hata sasa walikuwa wakiniomba, majuzi
tuliteketeza kiasi kama cha hekari tano za bangi maeneo ya milimani, kwa hiyo
kwa sasa hawaipati inawaumiza zaidi.
“Kikubwa tunaendelea kuwapatia elimu kwamba
bangi kwao si kitu kizuri, tutatafuta mbadala na kwa vile wameniomba nikutane
nao hilo nalo tutaliweka vizuri.
“Naamini vipo vitu mbadala wanavyoweza
kutumia badala ya bangi, mnawaona wanalalamika kwa sababu hawaipati. Tunajua ni
wawindaji wanakimbia na kupita maeneo magumu ndio maana wanaihitaji ili iwatoe
nishai, ukweli ni kwamba jambo hilo hatuwezi kuliruhusu,” alisema.
Wakati watu hao takribani 200 kutoka jamii ya
Kihadzabe wakiomba kupelekewa tani mbili za bangi, katika siku za hivi karibuni
baadhi ya wabunge waliomba zao hilo liruhusiwe kuwa la kibiashara ili
kuwaongezea kipato zaidi wakulima na wauzaji wa bangi.
Chakula kikuu cha jamii hiyo ni mizizi,
matunda pori, asali na nyama huku asali ikiwa ni miongoni mwa vitu
vinavyopendwa zaidi na jamii hiyo.
Namna wanavyoitumia mizizi hiyo kwa chakula;
wanakula kama ilivyo au kuichoma na ladha yake ni kama muhogo au viazi na
mizizi hiyo huwa na ukubwa kama wa mguu wa mtu mzima.
Matunda yao makuu ni kwantlanabe, kalahar,
kongolobi na ubuyu ambayo husagwa kwenye jiwe na unga wake husongwa kama ugali
na kuchanganywa na asali.
Vyakula vyao vinavyotegemea asili yao
haviwapi fursa ya kutumia mafuta, nyanya, kitunguu, sukari au kutumia vinywaji
vya viwandani, isipokuwa chumvi.
Wanyama wanaopendwa zaidi na Wahadzabe ni
pofu, nyani, tumbili, digidigi na twiga.
No comments