Maalim Seif : Tundu Lissu Hajapoteza Muelekeo, Akili Yake Ipo Timamu
Katibu
Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, ameeleza maendeleo
ya afya ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), baada ya
kumtembelea hospitalini Nairobi, Kenya.
Akihojiwa
na Redio ya Idhaa ya Kiswahili Deutsche Welle (DW) ya Ujerumani jana, Maalim
Seif alisema Lissu anaendelea vizuri na hajapoteza mwelekeo.
“Jana
(juzi) nilimtembelea Lissu na nilipata moyo sana, kwa kweli anaendelea vizuri
ukizingatia mtu ambaye alipigwa risasi zaidi ya 30, anapata nafuu haraka
haraka.
“Bado
hajapoteza mwelekeo akili yake ipo timamu, ametuhakikishia haya yaliyotokea
hayatamrudisha nyuma katika kuwatetea wanyonge.
“Anazungumza
vizuri, yuko makini sana anajua anachokisema na mimi nimepata moyo jinsi
nilivyomuona,” alisema Maalim Seif.
Alisema
kutokana na mambo yanayoendelea nchini, lazima kuwapo na mjadala wa
taifa kuona tumekosea wapi na kujirekebisha.
“Mambo
kama haya kutokea Tanzania ni jambo ambalo kila Mtanzania lazima aingiwe na
wasiwasi kwa sababu hakuna hata mmoja na hasa mwanasiasa ambaye ana usalama wa
maisha yake.
“Kama
taifa tuzungumze kuona tumekosea wapi na kujirekebisha,” alisema.
Kuhusu
uchunguzi wa tukio hilo, alisema hata kama vyombo vya dola vya ndani
vitafanya si aibu kwa nchi kutafuta msaada kwa wengine.
“Yako
mambo mengine yaliyotokea huko nyuma na bado hatujaaambiwa yalikwenda vipi,
tunaambiwa tu uchunguzi unaendelea. Ni vizuri wananchi waone matokeo ya
uchunguzi huo…si aibu kwa nchi kutafuta msaada kwa wengine,” alisema.
Lissu
alipigwa risasi zinazokadiriwa kufikia 32, Septemba 7, mwaka huu, alipokuwa
akirejea nyumbani kwake Area D mjini Dodoma baada ya kutoka kuhudhuria kikao
cha Bunge na kujeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake.
No comments