WAZIRI MKUU: RAIS HAJATANGAZA KUFUTWA KWA VYAMA VYA UPINZANI
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais, Dkt. John Magufuli hajawahi kutangaza ama kutoa kauli ya kufutwa kwa vyama vya siasa nchini.
Ametoa kauli hiyo
leo (Februari, 2, 2017) Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la Kiongozi
wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman Mbowe katika kipindi cha
maswali kwa Waziri Mkuu.
Katika swali lake
Mheshimiwa Mbowe alisema Rais Dkt. Magufuli alinukuliwa akisema
atahakikisha anafuta vyama vyama vya upinzani na ifikapo mwaka 2020 hakuna
upinzani nchini.
Pia Mheshimiwa
Mbowe alitaka kujua nini kauli ya Serikali kuhusu kunyimwa dhamana kwa Mbunge
wa Arusha Mjini, Mheshimiwa Godbless Lema ambaye anashikiliwa kwa muda miezi
mitatu.
Mbali na Mheshimiwa
Lema, pia kiongozi huyo alitaka kujua kuhusiana na kufungwa kwa Mbunge wa
Kilombelo, Mheshimiwa Peter Lijualikali pamoja na madiwani sita wa chama hicho
ambao wamefungwa na viongozi wengine 215 wanakabiliwa na kesi mbalimbali.
“Kwanza nataka
nikanushe kwamba Mheshimiwa Rais hajawahi kutangaza kuvifuta vyama vya
upinzani. Pia Watanzania wote wanajua nchi hii inaongozwa kwa sheria, kanuni na
taratibu i,” amesema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu ameongeza
kuwa “tunajua katika kuendesha nchi tunaendesha kwa mihimili mitatu ipo
Serikali, Mahakama na Bunge na hakuna mhimili unaoweza kuuingilia mhimili
mwingine,”.
“Pia Watanzania
wote wanajua kwamba jambo lolote ambalo lipo Mahakamani haliwezi kuzungumzwa
mahali pengine popote, hivyo siwezi kutumia nafasi hii kuzungumzia mambo yote
yanayoendelea chini ya sheria na yaliyo mahakamani,” amesema.
Wakati huo huo;
Waziri Mkuu amewahakikishia Watanzania kwamba suala la upungufu wa sukari
halitatokea nchini kwa sababu viwanda vya ndani vinaendelea kuzalisha na hadi
mwishoni mwa Januari vilifikia asilimia 86 ya uzalishaji.
“Hadi kufikia
mwishoni mwa msimu wa uzalishaji ambao ni mwezi Machi, tunaweza kuwa tumefikia
malengo na kama itajitokeza upungufu Serikali itatafuta namna nzuri ya kupata
sukari kwa kushirikiana na wenye viwanda nchini,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa
kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mvomero, Mheshimiwa Suleiman Sadiq
aliyetaka kujua hali ya sukari ilivyo nchini kwa sasa na hatua gani zinazochukuliwa
na Serikali ili kunusuru hali ya uhaba wa sukari isijitokeze.
No comments