UTOAJI TAARIFA ZA MIRADI YA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA UMMA UNAVYOSAIDIA KUPAMBANA NA RUSHWA
Na
Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Serikali
imeweka kipaumbele kikubwa katika ujenzi
wa miundombinu ya Umma kwani ni muhimu
kuwa na miundombinu mizuri na bora ili kutoa huduma bora na kurahisisha
ufanyaji kazi hivyo kuharakisha maendeleo ya nchi katika nyanja zote muhimu
zikiwemo za biashara, utalii na mawasiliano.
Matumizi
makubwa ya fedha za Serikali yanatumika katika ujenzi wa miundombinu ya Umma
ambapo matumizi hayo yanahusisha karibu asilimia 53 ya Bajeti nzima ya nchi.
Miradi
ya ujenzi wa miundombinu ya Umma inayoelezewa hapa ni ile ambayo inajengwa kwa
fedha za Serikali kwa ajili ya matumizi ya wananchi wote ikiwemo ya barabara,
hospitali na vituo vya afya,shule na vyuo,nyumba za kuishi pamoja na ofisi
mbalimbali.
Ingawa
Serikali inajitahidi kuhakikisha nchi inakuwa na miundombinu bora
itakayochochea maendeleo, lakini jitihada hizo zimekuwa zikikwamishwa na
changamoto mbalimbali zinazojitokeza pindi mradi husika unavyoanza kwani
wahusika hawatumii fedha kama zilivyopangwa na badala yake wanafanya kwa
makadirio ya chini na kufanya ujenzi kutokuwa imara.
Hali
hiyo inasababisha Serikali kupata hasara kwa kupoteza fedha nyingi na kuambulia
kubaki na majengo yasiyo na viwango ambayo mwisho wake hushindwa kutumika na
kuilazimu Serikali kuanza upya ujenzi husika.
Kwa
kuwa Serikali hii ni sikivu na imejipanga kuhakikisha nchi inafika katika
uchumi wa kati basi mambo hayo hayana nafasi na hayawezi kutokea tena katika
nchi hii watu kuachiwa huru kutumia vibaya fedha za Umma zinazotolewa kwa ajili
ya ujenzi wa miundombinu.
Kwa
kuhakikisha hilo,Serikali kupitia Baraza la Ujenzi la Taifa (NCC) chini ya
Mkakati wa Kukuza Uwazi na Uwajibikaji katika Sekta ya Ujenzi Tanzania
(CoST-Tanzania) imejipanga kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika sekta hiyo
ili kuondokana na rushwa pamoja na ubadhilifu wowote wa fedha za Umma
zinazotolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hiyo.
Mkakati
huo unalengo la kupambana na rushwa, usimamizi mbaya katika ujenzi pamoja na
changamoto zingine zinazopelekea ubadhilifu wa fedha zinazotengwa kwa ajili ya
miundombinu ya Umma kwa kukusanya taarifa za miradi hiyo ya ujenzi ili kuhakikisha kama thamani ya miundombinu
iliyojengwa inalingana na thamani ya fedha iliyotolewa kwa ajili ya ujenzi
husika.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,(Ujenzi), Mha. Joseph
Nyamuhanga alikaririwa akisema kuwa “Sekta ya Ujenzi ni sekta moja wapo
inayoonekana kukithiri kwa rushwa duniani kwa sababu takribani asilimia 10 hadi
30 ya Bajeti yake inapotea kwa njia ya rushwa na usimamizi mbaya hivyo ili
kuondoa dhima hii ni lazima kukusanya na kutoa taarifa kwa wananchi juu ya
ujenzi wa miundombinu hiyo”.
Mha.
Nyamuhanga aliongeza kuwa ni muhimu CoST-Tanzania ikapewa hadhi ya kujitegemea
na kuwa na madaraka yake kwani ni kitengo ambacho ni muhimu na kinafanya kazi
kubwa ya kuchochea uwepo wa uwazi na uwajibikaji katika miradi ya ujenzi.
Akifungua
mkutano wa wadau wa ujenzi kutoka nchi mbalimbali uliofanyika Jijini Dar es
Salaam hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
(Uchukuzi), Mha. Leonard Chamuriho alisema rushwa inazungumzwa sana katika
suala la ujenzi wa miundombinu ya umma hivyo huu ni wakati wa kuweka wazi
taarifa za ujenzi wa miundombinu hiyo ili wananchi waelewe kinachoendelea
katika miradi inayotumia fedha zao.
Aliongeza
kuwa kufanya hivyo kutaisaidia Serikali kupambana na rushwa na hivyo kufuta
kabisa taswira ya rushwa katika miradi hiyo kwani msimamo wa Serikali ni
kuhakikisha thamani ya fedha inazingatiwa.
Maendeleo
ya nchi yanachangiwa na wananchi wenyewe kwa njia ya ukusanyaji wa kodi na
ushuru mbalimbali hivyo hata miundombinu ya umma inajengwa kwa kutumia fedha za
wananchi zinazopatikana kwa njia ya ukusanyaji mapato.
Hivyo,
ili kuifanya Serikali kuwa na taswira nzuri kwa wananchi wao pamoja na
kuwafanya wananchi kuiamini Serikali yao ni vizuri kuwapa taarifa juu ya
matumizi ya fedha hizo wanazozikusanya.
Kuwapa
taarifa wananchi juu ya miradi mbalimbali haswa ya ujenzi wa miundombinu
kutaamsha ile hali ya watu kuona umuhimu wa kulipa kodi kwa sababu watajua
matumizi ya fedha wanazozikusanya.
Taarifa
hizo pia zitaendeleza uwajibikaji na uwazi katika ujenzi wa miundombinu hiyo
hivyo kupunguza vitendo vya rushwa,kujenga miundombinu inayoendana na thamani
ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi husika pamoja na kujenga miundo mbinu
bora na imara.
Kwa
upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki
amesema kuwa shughuli inayofanywa na CoST- Tanzania inalenga kuimarisha uwazi
katika sekta ya ujenzi kwa kutoa taarifa juu ya ujenzi wa miundombinu ya Umma
kitu ambacho kitasaidia kutambua uwezo, akiba pamoja na ufanisi wa majengo
hayo.
"Kazi
inayofanywa na CoST- Tanzania ni fursa kwa Serikali na Umma kwa ujumla
kufuatilia jinsi fedha za Umma zinavyotumika katika ujenzi wa miundombinu
ambapo ukweli na uwazi wa taarifa zinazokusanywa zitasaidia katika kupunguza
rushwa na kuboresha usimamizi wa miundombinu hiyo, " alisema Waziri
Kairuki.
Nae
Mwenyekiti wa CoST-Tanzania, Mha. Kazungu Magili alieleza kuwa utoaji wa
taarifa hizo kwa Umma kuhusiana na miradi ya ujenzi ya Umma itaruhusu umma
kujua hali ya miradi mbalimbali hivyo kuifanya Serikali kuwa na sifa nzuri
mbele ya wananchi.
CoST-Tanzania
imejipanga kufanya tathmini ya miradi ya ujenzi isiyopungua kumi ikiwa ni
pamoja na ujenzi wa madaraja, majengo yaliyojengwa na Wakala wa Majengo
Tanzania (TBA) hasa ujenzi mpya wa hosteli
za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pia majengo yanayojengwa na Mfuko wa
Taifa wa Hifadhi za Jamii (NSSF ) pamoja na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Ni
muhimu kwa Serikali kupitia miradi yote iliyojengwa na inayoendelea kujengwa
kwa kutumia fedha za Umma ili kugundua thamani halisi ya majengo hayo na kutoa
taarifa kwa wananchi.
Jambo
hili pia litasaidia vyombo husika vya kisheria kuwachukulia hatua watu wote
walioshiriki kutumia vibaya fedha za wananchi kwa kujenga miundombinu iliyo
chini ya kiwango au isiyoendana na thamani ya fedha iliyotolewa kwa ajili ya
ujenzi husika.
No comments