YAFAHAMU MAMBO YANAYOMLETA WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA CHINA NCHINI TANZANIA
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje
wa China nchini
Waziri wa Mambo ya Nje wa
Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. WANG Yi anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi
nchini tarehe 09 Januari 2017. Mhe. Waziri Wang Yi atapokelewa na mwenyeji wake
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt.
Augustine Mahiga.
Madhumuni ya ziara hiyo ni kukuza mahusiano mazuri na ya
kihistoria baina ya China na Tanzania ambayo yamedumu kwa zaidi ya miaka
hamsini tangu kuanzishwa kwake pamoja na
kuangalia maeneo mapya ya ushirikiano wa kiuchumi baina ya Tanzania na China.
Wakati wa ziara hiyo Mhe. Wang
Yi atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli kwa lengo la kumsalimia.
Aidha, Mhe. Wang Yi atafanya
mazungumzo rasmi na Mhe. Dkt. Mahiga kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano
baina ya Tanzania na China na ushirikiano wa kimataifa.
Itakumbukwa kwamba, Desemba
2015 kweneye Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika na China, China iliichagua
Tanzania kuwa miongoni mwa nchi nne Barani Afrika zitakazowezeshwa kupiga hatua
kwenye maendeleo ya viwanda. Kupitia mpango huo inatarajiwa viwanda takriban
200 vitajengwa au kuwekezwa nchini kutoka China kabla ya mwaka 2020.
Mpango huu unaenda sambamba na
Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2016/2020 na pia ahadi za Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Joseph Magufuli wa kujenga Tanzania ya
viwanda. Ni matarajio yetu kuwa, Watanzania takriban laki mbili watanufaika na
ajira kupitia mpango huu mahsusi wa kuendeleza viwanda.
Mbali na mpango wa uendelezaji
wa viwanda, viongozi hawa wawili watazungumzia miradi mingine ya miundombinu
ambapo China imeahidi kuisadia Tanzania ikiwa ni pamoja na maboresho makubwa ya
Reli ya TAZARA; Ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo pamoja na ujenzi wa Reli ya Kati.
Aidha, Mhe. Wang anatarajiwa
kuzungumza na Mwenyeji wake kuhusu masuala ya ushirikiano wa kimataifa ikiwa ni
pamoja na mageuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo China inaunga
mkono msimamo wa Afrika na wa Tanzania wa kutaka Afrika ipewe viti viwili vya
kudumu kwenye Baraza hilo na kura ya turufu.
Vilevile viongozi hao
watazungumzia masuala ya amani na usalama katika eneo la Afrika Mashariki
pamoja na eneo la Bahari ya Kusini mwa China.
Mazungumzo hayo yatafuatiwa na
Mkutano wa Mawaziri na Vyombo vya Habari (Joint Press Conference) ambapo
wataeleza makubaliano waliyofikia kwenye mazungumzo yao.
Imetolewa
na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dar
es Salaam
05
Januari, 2017
No comments