KUTOKA MASASI: MHE MAJALIWA AMEAGIZA MAOFISA WANNE WASWEKA RUMANDE KWA UPOTEVU WA KOROSHO
WAZIRI
Mkuu, Kassim Majaliwa, amemwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Zuberi
Mwombeji awakamate maofisa wanne wa Chama Kikuu Cha Ushirika (MAMCU) na
kuhakikisha wanapelekwa Masasi chini ya ulinzi wa Polisi kujibu tuhuma za
upotevu wa tani 2, 138 za korosho.
Kufuatia
agizo hilo, Polisi imewatia mbaroni watuhumiwa hao na juzi walipandishwa katika
karandinga la jeshi hilo na kupelekwa Masasi. Maofisa hao ni Kaimu Meneja Mkuu
Chama Kikuu cha Ushirika cha Masasi (MAMCU), Kelvin Rajab na Meneja Tawi wa MAMCU,
Lawrence Njozi.
Wengine
ni wakurugenzi wa kampuni ya YURAP ya Masasi inayohusika na uhifadhi wa mazao
kwenye maghala, Yusuph Namkukula na Ramadhani Namakweto.
Majaliwa
alifikia uamuzi huo juzi jioni kwenye kikao alichokiitisha Songea mjini baina
ya watendaji kutoka Bodi ya Korosho Tanzania, MAMCU, wamiliki wa ghala la
BUCO-Masasi na kikundi cha wakulima sita waliowawakilisha wenzao kutoka vyama
vya msingi (AMCOS) za wilaya za Mtwara na Masasi.
Katika
kikao hicho, Majaliwa alitaka maelezo ya kina ni wapi zilipo tani 2,138 za
korosho wakati taarifa waliyompa viongozi hao ilionesha waliuza korosho zote na
hakuna hata kilo moja ambayo haijanunuliwa katika mnada wa tano uliofanyika
Novemba 10, mwaka jana.
Kaimu
Meneja Mkuu wa MAMCU, Kelvin Rajab alikiri mbele ya Waziri Mkuu kwamba korosho
zote ziliuzwa na zilishalipwa na wanunuzi wa mnada wa tano lakini akadai
hakupewa taarifa ya kukosekana kwa kiasi hicho cha korosho. Naye mmiliki wa
ghala la BUCO, Ramadhan Namakweto alikiri kupokelewa kwa korosho hizo ghalani
kwake lakini akashindwa kutoa maelezo ni kwa nini hazionekani.
“Tangu
mnada wa tano, mmekwishafanya minada mingine mitano hadi kufikia mnada wa 10.
Kama kweli hizo korosho zipo ghalani, ni kwa nini za hawa wakulima hazijatolewa
ghalani na kuuzwa katika minada iliyofuata huku taarifa yenu ya fedha ikionesha
kuwa mlishazipokea na kuziuza?” alihoji Waziri Mkuu bila kupata majibu ya
kueleweka.
Tuhuma
zinazowakabili maofisa hao wanne ni kuwalipa kilo pungufu ya zile
zilizowasilishwa ghalani wakulima wa korosho katika wilaya ya Masasi na
kutowapa maelezo yoyote juu ya upungufu huo.
Mfano
wa suala hilo ni kufanya makato ya unyaufu kwa wakulima wa chama cha msingi
CHAMALI kinyume na maagizo ya Serikali. Nyingine ni kutowalipa fedha kwa wakati
wakulima waliouza korosho kwenye mnada wa tano wa Novemba 10, 2016 na kutokutoa
maelezo yoyote licha ya kuwa MAMCU ilishauza korosho hizo kwenye minada
iliyofuatia na kupokea malipo.
Tuhuma
nyingine ni kutopelekwa mnadani kwa makusudi kwa tani 2,138 za korosho zilizokuwa
katika maghala ya Mtandi na BUCO tangu Novemba 11, mwaka jana; kutokutolewa
taarifa ya kuwepo korosho hizo kwa mamlaka husika na kuwasababishia hasara
wananchi.
Dai
jingine linalowahusu maofisa hao ni kushindwa kufuatilia malipo ya korosho ya
tani 1,156,262 ambazo ziliuzwa kwenye mnada wa 10 uliofanyika Desemba 21, 2016.
Korosho hizo zilinunuliwa na Maviga East Africa (tani 503,297); Machinga
Transport (tani 104,200); Tastey (319,576) na Saweya Impex (tani (229,189).
Kutokana
na mapungufu hayo, Majaliwa aliagiza watu hao wapelekwe Masasi chini ya ulinzi
ili uchunguzi ufanyike.
Waziri
Mkuu pia alimuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye
ukaguzi wa hesabu za MAMCU na kujiridhisha kiasi cha korosho kilichonunuliwa;
fedha zilizolipwa na kuingia akaunti za MAMCU; kiasi cha fedha zilizolipwa kwa
vyama vya msingi na wananchi kwa ulinganifu na bei ya korosho kwa kila mnada
husika.
Awali,
wakisoma risala yao kwa Waziri Mkuu, wakulima walisema wana kero nyingi kama
vile kutolipwa fedha zao kwa wakati, kutoeleweka mahali zilipo korosho ambazo
walishaziuza kwa MAMCU, kukatwa makato ya unyaufu ambayo Serikali ilikwishapiga
marufuku na kutosikilizwa malalamiko yao na viongozi wa MAMCU pamoja na
viongozi wa mkoa na wilaya.
“Makubaliano
yalikuwa ni kwamba mkulima atapewa fedha yake siku sita baada ya mnada
kufanyika lakini hivi sasa baadhi yetu tumeuza korosho tangu Oktoba, mwaka jana
lakini hadi imefika Januari hii bado hatujalipwa.
Pia
kuna makato yaliyoondolewa kwenye mfumo, kwa mfano unyaufu lakini wao
wameyaacha na unapoenda kuuza wanahesabu na kukukata kuwa utalipia gharama za
unyaufu,” alisema msoma risala Sylvester Mtimbe ambaye pia ni mkulima kutoka
AMCOS ya Chiungutwa.
Wakulima
hao wa korosho kutoka Masasi mkoani Mtwara walikutana Januari 3,mwaka huu
katika kijiji cha Chiungutwa na kuazimia kuwa wangeandamana hadi Dar es Salaam
wawasilishe kilio chao kwa Waziri Mkuu au kwa Rais John Magufuli.
Kwa
kutambua umbali uliopo kutoka Masasi hadi Dar es Salaam na kwamba yeye (Waziri
Mkuu) hakuwepo katika siku waliyopanga kwenda huko, Waziri Mkuu aliamua kuwaita
wakulima hao wamfuate Songea ambako alikuwa na ziara ya kikazi ya siku nne.
Chanzo-Habarileo
No comments