ATAKAYEUGUA KIPINDUPINDU AFIKISHWE MAHAKAMANI, DC SINGIDA
Watu wawili wakazi wa jimbo la Singida
Kaskazini mkoani Singida, wamefariki dunia baada ya kuugua ugonjwa hatari wa
Kipindupindu unaotokana na uchafu.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi
jana ofisini kwake, Mkuu wa wilaya ya Singida, Elias Tarimo, alisema Novemba,
26 mwaka huu, ugonjwa huo wa Kipundupindu ulibainika katika vijiji vya Merya na
Msange jimbo la Singida kaskazini.
Hata hivyo, alisema kuwa ilichukua muda
mrefu mno mamlaka zinazohusika kutoa taarifa ya ugonjwa huo, kitendo
kilichochangia idadi ya wagonjwa kuongezeka na kufikia 30.
“Urasimu huu umesababisha hatua stahiki za
kudhibiti ugonjwa huu, kuchelewa kuchukuliwa na hivyo kuchangia wananchi wawili
kupoteza maisha. Kwa sasa tumebakiwa na wagonjwa sita kambi ya Merya na Msange
wapo watatu,” alisema Tarimo.
Mkuu huyo wa wilaya, alisema baada ya
kupata taarifa hizo kwa kuchelewa, hawakulala walipiga kampeni ya nguvu
kuhimiza usafi wa mazingira, matumizi bora ya vyoo na kuchemsha maji kwa ajili
ya matumizi ya nyumbani.
“Aidha, wataalam walipima maji ya visima 14
yanayotumiwa na wananchi wa vijiji hivyo, na 12 kubainika vina vidudu
vinavyochangia ugonjwa wa kipindu pindu. Baada ya kugundua hivyo, tumepiga
marufuku maji ya visima hivyo kutumika,” alisema.
Akifafanua, alisema wamewaelekeza wananchi
kutumia maji ya bomba na wamechukua mashine kubwa ya kupampu maji kutoka kijiji
cha Sagara.
“Mashine hii tumeisimika na itasambaza maji
ya bomba katika vijiji hivyo vya Msange na Merya. Hatujaishia hapo, tunaendelea
kuwahimiza wananchi kutumia vidoge vya waterguird kwa ajili ya kutibu maji yawe
safi na salama. Vile vile tanawahimiza kutumia vyoo na kuacha tabia ya
kujisaidia ovyo kwenye vichaka,” alisema.
Katika hatua nyingine, Tarimo alisema kuwa
baada ya kufanya kampeni ya kuhimza usafi, mwananchi yoyote atakayeugua
Kipindupindu, atatibiwa na akipona, mara moja atafikishwa mahakamani, kujibu
tuhuma ya kutaka kujiuawa kwa makusudi.
Wakati huo huo, katika kuchukua hatua
kudhibiti Kipindupindu, Manispaa ya Singida imechukua hatua mbalimbali, ikiwemo
ya kupiga marufuku wafanyabiashara wa matunda, kumenya matunda. Imeagizwa kuwa
matunda yote yaliwe nyumbani baada ya kuoshwa vizuri kwa maji.
Pia kila kaya imeagizwa kutumia vyoo bora
na kunawa mikono kwa sabuni kabla ya kula chakula na baada ya kutoka chooni.
Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Bravo Kizito
Lyapembile, amesema mtu ye yote akikamatwa kwa kuchafua mazingira, atatozwa
faini kati ya shilingi 30,000 na 300,000.
Na Nathaniel Limu, Singida
No comments