RC MAKONDA ASHAURI WANAOSOMESHWA MASOMO YA AFYA KWA MKOPO KUFANYA KAZI HOSPITALI ZA UMMA KWA MIAKA ISIYOPUNGUA MITATU.
Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Wanafunzi wanaosomea masomo ya afya kwa mkopo wa Serikali watakiwa kufanya kazi kwa miaka isiyopungua mitatu katika hospitali za umma kabla ya kwenda sehemu zingine.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda alipotembelea Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi kilichopo eneo la Mloganzila, Mkoani humo kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya ujenzi wa chuo hicho.
Mhe. Makonda amesema kuwa wanafunzi wanaosoma sekta ya afya kwa mikopo wanatumia Bajeti kubwa ambapo mwisho wa siku wanaondoka bila kuwatumikia wananchi hivyo, ameishauri Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuweka sheria kwa wanafunzi wanaosomea masomo hayo kwa mkopo kupewa sharti la msingi la kufanya kazi katika hospitali za umma kwa miaka isiyopungua mitatu.
“Tukiweka Sheria hiyo itaisaidia Serikali kutatua tatizo la upungufu wa watumishi wa afya kama ambavyo Serikali ilivyoona tatizo hili na ikaamua kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga chuo hiki ambacho kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 15,000 hivyo, ninaamini chuo hiki kitaondoa kabisa tatizo hilo,”alisema Mhe. Makonda.
Mhe, Makonda ameupongeza uongozi wa chuo hicho kwa kutenga eneo kwa ajili ya viwanda vya dawa na vifaa tiba pamoja na eneo litakalotumika kujenga kituo kikubwa cha utafiti wa masuala ya sayansi hivyo ameahidi kusaidiana nao kwa hali na mali katika kuhakikisha ujenzi wa chuo hicho unakamilika.
Naye Kaimu Makamo Mkuu wa Chuo hicho (Muhimbili), Eligius Lyamula amesema kuwa Serikali iliamua kutoa kiwanja chenye ukubwa wa hekari 3800 kwa ajili ya kupanua shughuli za chuo na kuweza kuzalisha wataalam wa kada mbalimbali za afya ili kuweza kutatua changamoto za afya zinazowakabili wananchi.
Ameongeza kuwa ujenzi wa eneo hilo ulianza kwa kujenga hospitali ya kisasa yenye uwezo wa kuweka vitanda 571 ambayo ilijengwa kwa mkopo wa riba nafuu kutoka Serikali ya Korea Kusini pamoja na fedha ya Serikali ya Tanzania hivyo hadi kukamilika kwake imegharimu jumla ya dola za kimarekani milioni 94,500,000.
“Hospitali hii inategemea kutoa huduma za kisasa pamoja na kutoa mafunzo kwa wanafunzi wanaosomea sekta ya afya, ujenzi ulikamilika mnamo Agosti 31 mwezi huu na inategemea kufunguliwa mwishoni mwa mwezi Januari mwaka 2017, kwa sasa wataalamu wanaendelea kuweka vifaa tiba na kufunga mifumo ya vifaa vya tehama ili kurahisisha kazi hospitalini humo,”alisema Lyamula.
Akiongelea kuhusu suala la watumishi, Lyamula amesema kuwa ili hospitali hiyo ifanye kazi kwa ufanisi itahitaji kuwa na watumishi 1300 ambapo hadi sasa kuna watumishi wa awali 928, watumishi 213 wanategemea kuhamishiwa kutoka hospitali mbalimbali nchini pia Serikali imeshatoa kibali cha kuajiri watumishi 50 hivyo huduma za afya katika hospitali hiyo zitakuwa za uhakika.
Aidha, amefafanua kuwa jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 510,696,243 zinaendelea kutafutwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu, madarasa, maktaba, majengo ya utawala, mabweni ya wanafunzi, kumbi za mikutano pamoja na maabara.
No comments