Breaking News

WATAALAM TIBA ASILI WATAKIWA KUFIKIRI KISAYANSI

Na WAF, MWANZA 
Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt Godwin Mollel, amewataka wataalam wa Tiba Asili kufikiri kisayansi ili matokeo ya dawa wanazo zizalisha ziwe na muelekeo wa kisayansi.

Dkt. Mollel amesema hayo Agosti, 31, 2024, wakati wa Kongamano la tatu la kisayansi la Tiba Asili lililofanyika jijini Mwanza kwa muda wa siku moja na kuwaleta pamoja Wataalam, Wadau na Watafiti wa Tiba Asili kutoka kote nchini. 

Amesema kuifanya huduma za Tiba Asili kuwa ya kisayansi Kutasaidia jamii kuondokana na dhana potofu dhidi ya Tiba Asili badala yake izingatie Tiba Asili iliyo thibitishwa na kupata ithibati kutoka mamlaka za kitafiti nchini.

"Tuifanye Tiba Asili kuwa ya kisayansi na tuwasaidie wananchi kuondokana na dhana potofu na tuione Tiba Asili kama sehemu yakusaidiana na Tiba zingine, tanzania imeendelea kupiga hatua kwenye matumizi ya Tiba Asili, mpaka sasa Hospitali saba za Rufaa za mikoa zimeendelea kutoa huduma Jumuishi ya Tiba Asili ikiwepo Sekouture ya mkoa wa Mwanza.", amesema, Dkt. Mollel.

Aidha, Dkt. Mollel, ameitaka Taasisi ya Taifa ya Uchunguzi (NIMR) na Mkemia Mkuu wa Serikali kufanya kazi kwa pamoja na kuharakisha ufanikishaji wa dawa zinazo ingia katika huduma jumuishi, huku akilitaka baraza Tiba Asili kupunguza urasimu ili mchakato wa ufuatiliaji wa vibali vya Tiba Asili uweze kukamilika kwa wakati.

Awali akitoa Salaam za Mganga Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi wa Huduma za Mama na Mtoto, kutoka Wizara ya Afya Dkt. Ahmad Makuani amesema mchango wa Tiba nchini umekuwepo tokea enzi na kabla ya ujio wa dawa za kisasa.

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili Tanzania Prof. Hamisi Malebo akitoa Salaam za Shukrani, ameiomba Serikali kuongeza fedha kwenye Taasisi ya Taifa ya Utafiti ili iweze kufanya utafiti kwa wingi.

"Uwezo wa NIMR ni kutafiti dawa zisizopungua 100 hivyo Serikali ikiiwezesha taasisi hii itakuwa msaada katika kuimarisha suala zima la tafiti." Amesema Dkt. Malebo.

No comments