TUME YA MADINI YAANZA UTEKELEZAJI WA DIRA YA MADINI YA MWAKA 2030
Mwanza:
Ikiwa ni utekelezaji wa Dira ya Madini ya Mwaka 2030 inayosema “Madini ni Maisha na Utajiri” sambamba na maelekezo ya Waziri wa Madini, Anthony Mavunde aliyoyatoa mapema jana kwa viongozi wa Tume ya Madini jijini Mwanza, leo viongozi wa Tume ya Madini wakiongozwa na Katibu Mtendaji Eng. Yahya Samamba wamekutana kwa ajili ya kuweka mikakati mbalimbali katika kuhakikisha lengo linafikiwa ikiwa ni pamoja na kutangaza fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini kuanzia kwenye uchimbaji, uchenjuaji, usafishaji, uyeyushaji na biashara ya madini.
Katika kikao hicho, Eng. Samamba amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na ubunifu wa hali ya juu ili mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa uendelee kukua na kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.
Yapanga mikakati kabambe ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Waziri Mavunde
Katika hatua nyingine, Eng. Samamba amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kuendelea kuimarisha udhibiti wa utoroshaji wa madini kwa kushirikiana kwa karibu na vyombo vya ulinzi na usalama.
Pia amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kuongeza kasi ya ukusanyaji wa maduhuli ili kuhakikisha lengo la makusanyo ya maduhuli kwa mwaka 2023-2024 la shilingi bilioni 882 linafikiwa mapema hivyo Sekta ya Madini kuendelea kuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.
Maelekezo yaliyotolewa awali na Waziri Mavunde kwa maafisa madini wakazi wa mikoa yalikuwa ni pamoja na kuendelea kufanya kazi kwa kufuata sheria na kanuni za madini, kuimarisha udhibiti wa utoroshaji wa madini kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama na kuongeza kasi ya utatuzi wa migogoro kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.
Maelekezo mengine yalikuwa ni pamoja na kuboresha mfumo wa taarifa za makusanyo ya maduhuli na kufanya kazi kwa kushirikiana na kubadilishana uzoefu.
No comments