Breaking News

WAZIRI WA KILIMO PROF MKENDA AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA MKURUGENZI MTENDAJI WA TBL NDG JOSE MORAN

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam

Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda leo tarehe 1 Disemba 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Bia cha Tanzaia Breweries Limited-TBL Ndg Jose Moran katika Ofisi ndogo za Wizara ya Kilimo Jijini Dar es salaam.

Waziri Mkenda ameipongeza TBL kwa kazi wanayoifanya nchini ikiwemo kutoa mikataba 4000 kwa wakulima wa mtama wilayani Kongwa katika mkoa wa Dodoma ambapo wamenunua mtama wa wakulima Tani 10,000.
“Utaratibu huo unawasaidia wakulima kwani hata mkulima mdogo anaweza kuingia kwenye kilimo cha kibishara kwenye mazao ya chakula kwahiyo na sisi kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko inapaswa kutumia utaratibu huo unaofanywa na TBL kwa wakulima, tena wafanye hivyo Wilayani Kongwa na kwingineko nchini kwa kuwa soko la Mtama limepatikana nchini Sudani Kusini” Amekaririwa Prof Mkenda

Waziri Mkenda amebainisha kuwa pamoja na mkataba wao kuwekwa lakini amemuomba mkurugenzi huyo wa TBL kuhakikisha kuwa ananunua mtama mwingi zaidi kwa wakulima.
Kuhusu zao la shairi ambalo TBL wana mkataba na wakulima 400 katika maeneo mbalimbali ikiwemo Wilayani Karatu ambapo mpaka sasa wamenunua  Tani 5000, Waziri Mkenda amefanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa TBL ili kuona uwezekano wa kununua Shairi kwa wakulima kwani walizasha kiasi kikubwa kuliko kilichoainishwa kwenye mkataba.

Kumekuwa na mazungumzo ya muda mrefu baina ya serikali na wazalishaji wa Bia nchini kuhakikisha kuwa wanatumia shairi inayolimwa nchini kwa ajili ya kutengeneza kimea ili wanywaji wa Bia wachangie mapato ya mkulima, Kodi na kuunda ajira kwa wananchi.
Waziri Mkenda amesema kuwa mazingira ya kikodi kwa wazalishaji wa Bia nchini kwa sasa ni mazuri hivyo ujenzi wa kiwanda cha Kimea kikijengwa kitaongeza soko la shairi kwa wakulima kutoka kwenye mkataba wa ununuzi wa Tani 5000 za shairi mpaka Tani 35,000  

“Unajua kila unapokunywa Bia nchini unakuwa umepeleka ajira nje ya nchi, unapeleka kodi kwa serikali ya nje na kupeleka fedha kwa wakulima wa nje ya nchi, Hivyo kuna kila sababu ya kuhakikisha kuwa tunakuwa na kiwanda cha Kimea hapa hapa nchini” Amesisitiza Waziri Mkenda.
Prof Mkenda amesema kuwa hiyo itakuwa hatua kubwa ya kuwainua wakulima wengi watakaojihusisha na kilimo hicho nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuno ya Bia (TBL) Ndg Jose Moran amemueleza mwenyeki wake ambaye ni Waziri wa Kilimo kuhusu Maendeleo ya Mkakati wa kuanza ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza Kimea kwani kimea kinachotumika nchini kinaagizwa nje ya nchi.

Mkurugenzi wa TBL amemuhakikishia Waziri Mkenda kuwa kati ya mwisho wa mwezi Januari, Februari mpaka Machi watakuwa tayari na tangazo linaloeleza ni lini shughuli ya ujenzi itaanza mwakani.

No comments